Mungu anamiliki kila kitu
Mungu anamiliki kila kitu duniani
Naye akambariki Abramu, akisema, “Abarikiwe Abramu na Mungu Aliye Juu Sana, Muumba wa mbingu na nchi. (Mwanzo 14:19)
Lakini Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, “Nimeinua mkono wangu kwa Bwana, Mungu Aliye Juu Sana, Muumba wa mbingu na dunia, na nimeapa (Mwanzo 14:22)
Mose akamjibu, “Nitakapokuwa nimetoka nje ya mji, nitanyoosha mikono yangu juu kumwomba Bwana. Ngurumo zitakoma na hapatakuwepo mvua ya mawe tena, ili upate kujua kuwa, nchi ni mali ya Bwana. (Kutoka 9:29)
Sasa kama mkinitii kikamilifu na kutunza Agano langu, basi ninyi mtakuwa mali yangu ya thamani kubwa miongoni mwa mataifa yote. Ijapokuwa dunia yote ni mali yangu, (Kutoka 19:5)
Mbingu, hata mbingu za juu sana, dunia na kila kitu kilichomo ndani yake, ni mali ya Bwana Mungu wako. (Kumbukumbu 10:14)
Ukuu na uweza, ni vyako, Ee Bwana, na utukufu na enzi na uzuri, kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani ni chako wewe. Ee Bwana, ufalme ni wako; umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote. “Lakini mimi ni nani, nao watu wangu ni nani, hata tuweze kukutolea kwa ukarimu namna hii? Vitu vyote vyatoka kwako, nasi tumekutolea tu vile vitokavyo mkononi mwako. Sisi ni wageni na wapitaji machoni pako, kama walivyokuwa baba zetu wote. Siku zetu duniani ni kama kivuli, bila tumaini. Ee Bwana Mungu wetu, kwa wingi wote huu ambao tumekutolea kwa kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina lako Takatifu, vimetoka mkononi mwako, navyo vyote ni mali yako. (1 Nyakati 29:11, 14-16)
Ni nani mwenye madai dhidi yangu ili nipate kumlipa? Kila kitu kilicho chini ya mbingu ni mali yangu. (Ayubu 41:11)
Zaburi ya Daudi. Dunia ni mali ya Bwana, na vyote vilivyomo ndani yake, ulimwengu, na wote waishio ndani yake, (Zaburi 24:1)
Kama ningekuwa na njaa, nisingewaambia ninyi, kwa maana ulimwengu ni wangu, pamoja na vyote vilivyomo ndani yake. (Zaburi 50:12)
Ee Mungu, inuka uihukumu nchi, kwa kuwa mataifa yote ni urithi wako. (Zaburi 82:8)
Mbingu ni zako, nayo nchi pia ni yako, uliuwekea ulimwengu msingi pamoja na vyote vilivyomo. (Zaburi 89:11)
Mkononi mwake mna vilindi vya dunia, na vilele vya milima ni mali yake. Bahari ni yake, kwani ndiye aliifanya, na mikono yake iliumba nchi kavu. (Zaburi 95:4-5)
Ee Bwana, jinsi matendo yako yalivyo mengi! Kwa hekima ulizifanya zote, dunia imejaa viumbe vyako. (Zaburi 104:24)
Kwa maana, “Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana.” (1 Wakorintho 10:26)
Mfano unaoonyesha umiliki wa Mungu
“Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama mtu aliyetaka kusafiri, naye akawaita watumishi wake na kuweka mali yake kwenye uangalizi wao. Mmoja akampa talanta tano, mwingine talanta mbili, na mwingine talanta moja. Kila mmoja alipewa kwa kadiri ya uwezo wake. Kisha yeye akasafiri. Yule aliyepewa talanta tano akaenda mara moja akafanya nazo biashara akapata talanta nyingine tano zaidi. Yule aliyepewa talanta mbili akafanya vivyo hivyo, akapata nyingine mbili zaidi. Lakini yule mtumishi aliyekuwa amepokea talanta moja, alikwenda akachimba shimo ardhini na kuificha ile fedha ya bwana wake. “Baada ya muda mrefu, yule bwana wa wale watumishi akarudi na kufanya hesabu nao. Yule mtumishi aliyepokea talanta tano akaja, akaleta nyingine tano zaidi. Akasema, ‘Bwana uliweka kwenye uangalizi wangu talanta tano. Tazama, nimepata faida ya talanta tano zaidi.’ “Bwana wake akamwambia, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu! Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’ “Yule mwenye talanta mbili naye akaja. Akasema, ‘Bwana, uliweka kwenye uangalizi wangu talanta mbili. Tazama nimepata hapa talanta mbili zaidi.’ “Bwana wake akajibu, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’ “Kisha yule mtumishi aliyepokea talanta moja akaja, akasema, ‘Bwana, nilijua kwamba wewe ni mtu mgumu, unayevuna mahali usipopanda na kukusanya mahali usipotawanya mbegu. Kwa hiyo niliogopa, nikaenda, nikaificha talanta yako ardhini. Tazama, hii hapa ile iliyo mali yako.’ “Bwana wake akajibu, ‘Wewe mtumishi mwovu na mvivu! Ulijua kwamba ninavuna mahali nisipopanda na kukusanya mahali nisipotawanya mbegu. Vyema basi, ingekupasa kuweka fedha yangu kwa watoa riba, ili nirudipo, nichukue ile iliyo yangu na faida yake. “ ‘Basi mnyangʼanyeni hiyo talanta, mkampe yule mwenye talanta kumi. (Mathayo 25:14-28)
Bwana hushikamanisha vitu vyote
Mwana ni mngʼao wa utukufu wa Mungu na mfano halisi wa nafsi yake, akivihifadhi vitu vyote kwa neno lake lenye uweza. Akiisha kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Aliye Mkuu huko mbinguni. (Waebrania 1:3)
Yeye alikuwepo kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja. (Wakolosai 1:17)
Mali mahususi anazomiliki Mungu
Ardhi
“ ‘Kamwe ardhi isiuzwe kwa mkataba wa kudumu, kwa sababu nchi ni mali yangu, nanyi ni wageni na wapangaji wangu. (Walawi 25:23)
Dhahabu na fedha
Pia ulichukua vito vizuri nilivyokupa, vito vilivyotengenezwa kwa dhahabu yangu na fedha yangu, ukajitengenezea navyo sanamu za kiume na ukafanya ukahaba nazo. (Ezekieli 16:17)
‘Fedha ni mali yangu na dhahabu ni mali yangu,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. (Hagai 2:8)
Wanyama
Kwa maana kila mnyama wa msituni ni wangu, na pia makundi ya mifugo juu ya vilima elfu. Ninamjua kila ndege mlimani, nao viumbe wa kondeni ni wangu. (Zaburi 50:10-11)
Mungu hudhibiti kila tukio
Bwana hudhibiti matukio yote duniani
Ukuu na uweza, ni vyako, Ee Bwana, na utukufu na enzi na uzuri, kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani ni chako wewe. Ee Bwana, ufalme ni wako; umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote. Utajiri na heshima vyatoka kwako; wewe ndiwe utawalaye vitu vyote. Mikononi mwako kuna nguvu na uweza ili kuinua na kuwapa wote nguvu, (1 Nyakati 29:11-12)
Bwana hufanya lolote apendalo, mbinguni na duniani, katika bahari na vilindi vyake vyote. (Zaburi 135:6)
Kura hupigwa kwa siri, lakini kila uamuzi wake hutoka kwa Bwana. (Mithali 16:33)
Hatua za mtu huongozwa na Bwana. Anawezaje basi mtu yeyote kuelewa njia yake mwenyewe? (Mithali 20:24)
...na akasema: “Lihimidiwe jina la Mungu milele na milele; hekima na uweza ni vyake. Yeye hubadili nyakati na majira; huwaweka wafalme na kuwaondoa. Huwapa hekima wenye hekima, na maarifa wenye ufahamu. (Danieli 2:20-21)
Bwana huruhusu hali ngumu kutokea
Ndipo ndugu zake wote waume kwa wake na kila mtu aliyemfahamu mwanzoni, wakaja wakala pamoja naye katika nyumba yake. Wakamfariji na kumtuliza moyo juu ya taabu yote Bwana aliyoileta juu yake, nao kila mmoja akampa kipande cha fedha na pete ya dhahabu. (Ayubu 42:11)
...ili kutoka mawio ya jua mpaka machweo yake, watu wapate kujua kwamba hakuna Mungu mwingine ila Mimi. Mimi ndimi Bwana wala hakuna mwingine. Mimi ninaumba nuru na kuhuluku giza, ninaleta mafanikio na kusababisha maafa. Mimi, Bwana, huyatenda haya yote. (Isaya 45:6-7)
Nani awezaye kusema nalo likatendeka kama Bwana hajaamuru? Je, si ni kwenye kinywa cha Aliye Juu Sana ndiko yatokako maafa na mambo mema? (Maombolezo 3:37-38)
Je, tarumbeta inapopigwa mjini kujulisha hatari, watu hawatetemeki? Mji upatwapo na maafa, je, si Bwana amesababisha? (Amosi 3:6)
Bwana hutumia kila hali kwa kusudi jema katika maisha ya wanaomcha
Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. (Warumi 8:28)
Mfano wa Bwana kuruhusu hali ngumu kwa ajili ya mema ya mwisho
Sasa, msihuzunike wala msijichukie wenyewe kwa kuniuza huku, kwa sababu ilikuwa ni ili kuokoa maisha ya watu ndiyo sababu Mungu alinituma niwatangulie ninyi. Kwa miaka miwili sasa imekuwepo njaa katika nchi, pia kwa miaka mitano ijayo hapatakuwepo kulima wala kuvuna. Lakini Mungu alinitanguliza mbele yenu ili kuhifadhi mabaki kwa ajili yenu katika nchi, na kuokoa maisha yenu kwa wokovu mkuu. “Kwa hiyo basi, si ninyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Alinifanya kuwa baba kwa Farao, bwana wa watu wa nyumbani mwake wote, na mtawala wa Misri yote. Sasa rudini haraka kwa baba yangu na mwambieni, ‘Hili ndilo mwanao Yosefu asemalo: Mungu amenifanya mimi kuwa bwana wa Misri yote. Shuka uje kwangu, wala usikawie. (Mwanzo 45:5-9)
Mtazamo wa mtu wa mwili juu ya kudhibitiwa kwa matukio
Nimeona kitu kingine tena chini ya jua: Si wenye mbio washindao mashindano au wenye nguvu washindao vita, wala si wenye hekima wapatao chakula au wenye akili nyingi wapatao mali, wala wenye elimu wapatao upendeleo, lakini fursa huwapata wote. (Mhubiri 9:11)
Matukio na vitu mahususi ambavyo Bwana hudhibiti
Bwana huongoza mioyo ya watu
Moyo wa mfalme uko katika mkono wa Bwana; huuongoza kama mkondo wa maji, popote apendapo. (Mithali 21:1)
Bwana anaweza kuwapa wanaomcha kibali mbele ya wengine
Bwana alikuwa pamoja naye, akamhurumia na kumpa kibali mbele ya msimamizi wa gereza. (Mwanzo 39:21)
Kwa muda wa siku saba waliiadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu kwa furaha, kwa sababu Bwana alikuwa amewajaza furaha kwa kubadilisha nia ya mfalme wa Ashuru kwamba awasaidie ujenzi wa nyumba ya Mungu, Mungu wa Israeli. (Ezra 6:22)
Naomba nipewe barua nipeleke kwa Asafu, mtunzaji wa msitu wa mfalme, ili anipe miti ya kutengeneza boriti kwa ajili ya malango ya ngome ya Hekalu, na ukuta wa mji, na makao yangu nitakapoishi.” Kwa kuwa mkono wenye neema wa Mungu wangu ulikuwa juu yangu, mfalme akanijalia ombi langu. Pia niliwaambia kuhusu mkono wenye neema wa Mungu wangu uliokuwa juu yangu, na kile mfalme alichokuwa ameniambia. Wakajibu, “Haya! Tuanze kujenga tena.” Kwa hiyo wakaanza kazi hii njema. (Nehemia 2:8, 18)
Mfano wa Waisraeli kuwateka nyara Wamisri
“Nami nitawapa hawa watu upendeleo mbele ya Wamisri, kwa hiyo mtakapoondoka nchini hamtaondoka mikono mitupu. Kila mwanamke Mwisraeli atamwomba jirani yake Mmisri na mwanamke yeyote anayeishi nyumbani kwake ampe vyombo vya fedha, dhahabu na nguo, ambavyo mtawavika wana wenu na binti zenu. Hivyo mtawateka nyara Wamisri.” (Kutoka 3:21-22)
Waisraeli wakafanya kama Mose alivyowaelekeza, nao wakawaomba Wamisri wawapatie vitu vya fedha, dhahabu na nguo. Basi Bwana alikuwa amewafanya Wamisri kuwa wakarimu kwa hawa watu, wakawapatia Waisraeli vile walivyotaka kwao; kwa hiyo wakawateka nyara Wamisri. (Kutoka 12:35-36)
Bwana huifanya mioyo ya baadhi ya watu kuwa migumu
Nami nitaufanya moyo wa Farao mgumu, naye atawafuatilia. Lakini nitajipatia utukufu kwa ajili yangu mwenyewe kupitia Farao na jeshi lake lote, nao Wamisri watajua kuwa mimi ndimi Bwana.” Kwa hiyo Waisraeli wakafanya hivyo. (Kutoka 14:4)
Lakini Sihoni mfalme wa Heshboni alikataa kuturuhusu kupita. Kwa kuwa Bwana Mungu wako alikuwa ameifanya roho yake kuwa ngumu na moyo wake kuwa mkaidi ili amweke kwenye mikono yenu, kama alivyofanya sasa. (Kumbukumbu 2:30)
Bwana hudhibiti tamaa ya moyo
Mara tatu kwa mwaka wanaume wako wote watakuja mbele za Bwana Mwenyezi, Mungu wa Israeli. Nitawafukuza mataifa mbele yako na kupanua mipaka ya nchi yako, wala hakuna mtu yeyote atakayeitamani nchi yako wakati unapokwenda mara tatu kila mwaka kuonana na Bwana Mungu wako. (Kutoka 34:23-24)
Bwana hudhibiti mataifa
Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi. (Matendo 17:26)
Lakini mtu wa Mungu akamjia na kumwambia, “Ee mfalme, haya majeshi kutoka Israeli kamwe usiyaruhusu yaende pamoja na wewe kwa kuwa Bwana hayuko pamoja na Israeli, wala hayupo pamoja na yeyote wa watu wa Efraimu. Hata kama ukienda na kupigana kwa ujasiri katika vita, Mungu atakufanya ukimbie mbele ya adui, kwa kuwa Mungu anao uwezo wa kusaidia au wa kuangusha.” Amazia akamuuliza yule mtu wa Mungu, “Lakini itakuwaje kwa zile talanta 100 za fedha nilizolipa kwa ajili ya haya majeshi ya Israeli?” Yule mtu wa Mungu akajibu, “Bwana aweza kukupa zaidi sana ya hizo.” (2 Nyakati 25:7-9)
“Ole kwa Ashuru, fimbo ya hasira yangu, ambaye mkononi mwake ana rungu ya ghadhabu yangu! Ninamtuma dhidi ya taifa lisilomjua Mungu, ninamtuma dhidi ya taifa linalonikasirisha, kukamata mateka na kunyakua nyara, pia kuwakanyaga chini kama matope ya barabarani. (Isaya 10:5-6)