Choyo

Choyo kinalaumiwa kama ibada ya sanamu inayozuia urithi katika Ufalme wa Mungu. Maandiko yanaonya juu ya asili yake ya uharibifu, yakionyesha jinsi kinavyoongoza kwenye uovu na unyonyaji, na hatimaye hukumu ya Mungu.

Amri ya kutokuwa na choyo

Lakini uasherati, usitajwe miongoni mwenu, wala uchafu wa aina yoyote, wala tamaa, kwa sababu mambo haya hayastahili miongoni mwa watakatifu. (Waefeso 5:3)
Kwa habari ya mambo haya mjue hakika kwamba: Msherati, wala mtu mwovu, wala mwenye tamaa mbaya, mtu kama huyo ni mwabudu sanamu, kamwe hataurithi Ufalme wa Kristo na wa Mungu. (Waefeso 5:5)

Choyo ni ibada ya sanamu

Kwa hiyo, ueni kabisa chochote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: yaani uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ulafi, ambayo ndiyo ibada ya sanamu. (Wakolosai 3:5)

Jihadharini na kila aina ya choyo

Ndipo Yesu akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.” (Luka 12:15)

Jizuie ikiwa una mwelekeo wa choyo

Uketipo kula chakula na mtawala, angalia vyema kile kilicho mbele yako, na utie kisu kooni mwako kama ukiwa mlafi. Usitamani vyakula vyake vitamu kwa kuwa chakula hicho ni cha hila. (Mithali 23:1-3)

Kristo anapokuwa shauku yetu, choyo si tatizo tena

Nani niliye naye mbinguni ila wewe? Dunia haina chochote ninachokitamani ila wewe. (Zaburi 73:25)

Mfano wa mtu anayemcha Mungu asiye na choyo

Kama mjuavyo, hatukuja kwenu kwa maneno ya kujipendekeza au maneno yasiyo ya kweli ili kuficha tamaa mbaya: Mungu ndiye shahidi yetu. (1 Wathesalonike 2:5)

Bwana huadhibu choyo

Kama mfano kwa watoto wake

Basi mambo haya yalitokea kama mifano ili kutuzuia tusiweke mioyo yetu katika mambo maovu kama wao walivyofanya. (1 Wakorintho 10:6)

Kile ambacho wenye choyo walitamani

Umati wa watu wenye zogo waliokuwa miongoni mwao walitamani sana chakula kingine, Waisraeli wakaanza kulia tena na kusema, “Laiti tungekuwa na nyama tule! Tunakumbuka wale samaki tuliokula huko Misri bila gharama, pia yale matango, matikitimaji, mboga, vitunguu, na vitunguu saumu. (Hesabu 11:4-5)

Mfano wa watu wenye choyo

Watu wakarukia zile nyara, wakichukua kondoo, ngʼombe na ndama, wakawachinja hapo juu ya nchi na kuwala, pamoja na damu. (1 Samweli 14:32)

Viongozi wenye choyo

Ni mbwa wenye tamaa kubwa, kamwe hawatosheki. Wao ni wachungaji waliopungukiwa na ufahamu; wote wamegeukia njia yao wenyewe, kila mmoja hutafuta faida yake mwenyewe. (Isaya 56:11)

Watu wenye choyo ni waovu

Nao kwa kuwa hawakuona umuhimu wa kudumisha ufahamu wa Mungu, yeye akawaachilia wafuate akili za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa. Wakiwa wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji, (Warumi 1:28-29)
Hujivunia tamaa za moyo wake; humbariki mlafi na kumtukana Bwana. Katika kiburi chake, mwovu hamtafuti Mungu, katika mawazo yake yote hakuna nafasi ya Mungu. (Zaburi 10:3-4)

Choyo kitawanasa wenye choyo

Haki ya wanyofu huwaokoa, bali wasio waaminifu hunaswa na tamaa mbaya. (Mithali 11:6)

Manabii wa uongo watautumia mwili wa Kristo kwa sababu ya choyo

Lakini pia waliinuka manabii wa uongo miongoni mwa watu, kama vile watakavyokuwako walimu wa uongo miongoni mwenu. Wataingiza mafundisho yasiyopatana na kweli kwa siri, hata kumkana Bwana wa pekee aliyewanunua, na hivyo kujiletea wenyewe maangamizi ya haraka. Hata hivyo, wengi watafuata njia zao za ufisadi, na kwa ajili yao njia ya kweli itatukanwa. Nao katika tamaa zao mbaya, walimu hawa watajipatia faida kwenu kwa hadithi walizotunga wenyewe. Lakini hukumu imekwisha kutangazwa dhidi yao tangu zamani, wala uangamivu wao haujalala usingizi. (2 Petro 2:1-3)
Wakiwa na macho yaliyojaa uzinzi, kamwe hawaachi kutenda dhambi. Huwashawishi wale wasio imara. Wao ni hodari kwa kutamani; ni wana wa laana! Wameiacha njia iliyonyooka, wakapotoka na kuifuata njia ya Balaamu mwana wa Beori aliyependa mshahara wa uovu. (2 Petro 2:14-15)

Kuna wale ambao hawatatosheka kamwe

“Mruba anao binti wawili waliao, ‘Nipe! Nipe!’ “Kuna vitu vitatu visivyotosheka kamwe, naam, viko vinne visivyosema, ‘Yatosha!’: (Mithali 30:15)

Watu wa kidini wanaweza kuwa na choyo

Watu wangu wanakujia, kama wafanyavyo, nao wanaketi mbele yako kama watu wangu na kusikiliza maneno yako, lakini hawayatendi. Kwa maana udanganyifu u katika midomo yao, lakini mioyo yao ina tamaa ya faida isiyo halali. (Ezekieli 33:31)

Mfano wa Bwana kuwaadhibu watu wenye choyo

Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Kibroth-Hataava, kwa sababu huko ndiko walipowazika watu ambao walitamani sana chakula kingine. (Hesabu 11:34)
Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akajiambia mwenyewe, “Bwana wangu amemwachia kirahisi sana Naamani, huyu Mwaramu, kwa kutokupokea kutoka kwake vile alivyovileta. Hakika kama Bwana aishivyo, nitamkimbilia na kupata kitu kutoka kwake.” Hivyo Gehazi akaharakisha kumfuatilia Naamani. Naamani alipomwona akikimbia kumwelekea, akashuka chini kutoka kwenye gari lake na kwenda kumlaki. Akauliza, “Je, mambo yote ni sawa?” Gehazi akajibu, “Mambo yote ni sawa. Bwana wangu amenituma nikuambie, ‘Vijana wawili kutoka kwa wana wa manabii wamenijia kutoka nchi ya vilima ya Efraimu. Tafadhali wape talanta ya fedha na mivao miwili ya mavazi.’ ” Naamani akasema, “Hakika, chukua talanta mbili za fedha.” Akamsihi Gehazi azipokee, kisha akafunga talanta mbili za fedha katika mifuko miwili pamoja na mivao miwili ya mavazi. Akawapa watumishi wake wawili mizigo hiyo, nao wakaibeba wakitangulia mbele ya Gehazi. Gehazi alipofika kwenye kilima, akavichukua vile vitu kutoka kwa wale watumishi na kuvificha ndani ya nyumba. Akawaaga wale watu, nao wakaondoka. Kisha akaingia ndani na kusimama mbele ya Elisha bwana wake. Elisha akamuuliza, “Gehazi, ulikuwa wapi?” Gehazi akajibu, “Mtumishi wako hakwenda popote.” Lakini Elisha akamwambia, “Je, roho yangu haikuwa pamoja nawe wakati yule mtu aliposhuka kutoka kwenye gari lake ili kukulaki? Je, huu ni wakati wa kupokea fedha au kupokea nguo, mashamba ya mizeituni, mashamba ya mizabibu, makundi ya kondoo na mbuzi, makundi ya ngʼombe, au watumishi wa kiume na wa kike? Ukoma wa Naamani utakushika wewe na wazao wako milele.” Kisha Gehazi akaondoka mbele ya Elisha, mwenye ukoma, mweupe kama theluji. (2 Wafalme 5:20-27)
Nyumba zao zitapewa watu wengine, pamoja na mashamba yao na wake zao, nitakapounyoosha mkono wangu dhidi ya wale waishio katika nchi,” asema Bwana. “Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa, wote wana tamaa ya kupata faida zaidi; manabii na makuhani wanafanana, wote wanafanya udanganyifu. (Yeremia 6:12-13)
Kwa hiyo nitawapa watu wengine wake zao, na mashamba yao kwa wamiliki wengine. Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa, wote wana tamaa ya kupata zaidi; manabii na makuhani wanafanana, wote wanafanya udanganyifu. (Yeremia 8:10)