Kusalitiwa kwa Yesu
Kisha mmojawapo wa wale kumi na wawili, aitwaye Yuda Iskariote, alikwenda kwa viongozi wa makuhani na kuuliza, “Mtanipa nini nikimtia Yesu mikononi mwenu?” Wakamlipa vipande thelathini vya fedha. (Mathayo 26:14-15)
Yuda, ambaye alikuwa amemsaliti Yesu, alipoona kuwa Yesu amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. Akasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.” Wakamjibu, “Hilo latuhusu nini sisi? Ni shauri yako.” Basi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga. Wale viongozi wa makuhani wakazichukua zile fedha wakasema, “Si halali kuchanganya fedha hizi na sadaka kwa sababu hizi ni fedha zenye damu.” Kwa hiyo baada ya kushauriana, waliamua kuzitumia kununulia shamba la mfinyanzi, liwe mahali pa kuzikia wageni. Hii ndiyo sababu lile shamba likaitwa Shamba la Damu hadi leo. Ndipo likatimia lile lililonenwa na nabii Yeremia, kwamba, “Walichukua vile vipande thelathini vya fedha, thamani aliyopangiwa na watu wa Israeli, wakanunulia shamba la mfinyanzi, kama vile Bwana alivyoniagiza.” (Mathayo 27:3-10)
Kisha Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, akaenda kwa viongozi wa makuhani ili kumsaliti Yesu kwao. Walifurahi sana kusikia jambo hili na wakaahidi kumpa fedha. Hivyo yeye akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti. (Marko 14:10-11)
Shetani akamwingia Yuda, aliyeitwa Iskariote, mmoja wa wale Kumi na Wawili. Yuda akaenda kwa viongozi wa makuhani na kwa maafisa wa walinzi wa Hekalu, akazungumza nao jinsi ambavyo angeweza kumsaliti Yesu. Wakafurahi na wakakubaliana kumpa fedha. (Luka 22:3-5)
(Basi Yuda alinunua shamba kwa zile fedha za uovu alizopata; akiwa huko shambani akaanguka, akapasuka na matumbo yote yakatoka nje. (Matendo 1:18)
Ndugu waliouzwa utumwani
Kwa hiyo wale wafanyabiashara Wamidiani walipofika pale, ndugu zake wakamtoa Yosefu kutoka kwenye lile shimo, na kumuuza kwa shekeli ishirini za fedha kwa wale Waishmaeli, ambao walimpeleka Misri. (Mwanzo 37:28)
Fedha zilizolipwa kwa ajili ya uaguzi
Wazee wa Moabu na wa Midiani wakaondoka, wakiwa wamechukua ada ya uaguzi. Walipokwenda kwa Balaamu, wakamweleza kile Balaki alikuwa amesema. (Hesabu 22:7)
Lakini Balaamu akawajibu, “Hata kama Balaki angenipa jumba lake la kifalme likiwa limejazwa fedha na dhahabu, singeweza kufanya kitu chochote kikubwa au kidogo ili kutenda kitu nje ya agizo la Bwana Mungu wangu. (Hesabu 22:18)
‘Hata ikiwa Balaki angenipa jumba lake la kifalme likiwa limejazwa fedha na dhahabu, nisingeweza kufanya kitu chochote kwa matakwa yangu, kikiwa kizuri au kibaya, kwenda kinyume na agizo la Bwana, nami imenipasa kusema tu kile Bwana atakachosema’? (Hesabu 24:13)
Fedha zilizotolewa ili kujaribu kuangamiza taifa la Wayahudi
Kama inampendeza mfalme, itolewe amri kuwaangamiza, nami nitaweka talanta 10,000 za fedha katika hazina ya mfalme kwa ajili ya watu watakaoshughulikia jambo hili.” Basi mfalme alichukua pete yake ya muhuri kutoka kwenye kidole chake na kumpa Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, adui wa Wayahudi. Mfalme akamwambia Hamani, “Baki na fedha yako na uwatendee hao watu utakavyo.” (Esta 3:9-11)
Mordekai akamwambia kila kitu ambacho kimempata, pamoja na hesabu kamili ya fedha ambazo Hamani aliahidi kulipa katika hazina ya mfalme kwa ajili ya maangamizi ya Wayahudi. (Esta 4:7)
Fedha zilizolipwa ili kumdhuru Samsoni
Baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika Bonde la Soreki aliyeitwa Delila. Viongozi wa Wafilisti wakamwendea yule mwanamke na kumwambia, “Umbembeleze ili upate kujua siri za nguvu zake zilizo nyingi na jinsi tutakavyoweza kumshinda ili tuweze kumfunga na kumtiisha. Nasi kila mmoja wetu tutakupa shekeli 1,100 za fedha.” (Waamuzi 16:4-5)
Delila alipoona kuwa amemweleza siri yake yote, akatuma ujumbe kwa viongozi wa Wafilisti na kusema, “Njooni tena mara nyingine, maana amenieleza siri yake yote.” Basi viongozi wa Wafilisti wakaja kwa Delila, wakiwa na fedha mikononi mwao. (Waamuzi 16:18)
Fedha zilizolipwa kwa ajili ya mauaji
Wakampa shekeli sabini za fedha kutoka hekalu la Baal-Berithi, naye Abimeleki akaitumia kuajiri watu ovyo wasiojali, wakawa ndio wafuasi wake. (Waamuzi 9:4)