Madeni

Maandiko yanahimiza kuepuka madeni, yakiyaona kama aina ya utumwa, na kusisitiza umuhimu wa kulipa tunachodaiwa. Mifano ya Biblia inaonyesha mzigo wa madeni na baraka ya kutokuwa na deni, ikisisitiza riziki ya Mungu na uwajibikaji wa kifedha.

Tunahimizwa tusiwe na madeni

Msidaiwe kitu na mtu yeyote, isipokuwa kupendana, kwa maana yeye ampendaye mwenzake, ameitimiza sheria. (Warumi 13:8)

Deni linalinganishwa na utumwa

Matajiri huwatawala maskini naye akopaye ni mtumwa wa akopeshaye. (Mithali 22:7)

Amri ya kutokuwa watumwa wa wengine

Mlinunuliwa kwa gharama; msiwe watumwa wa wanadamu. (1 Wakorintho 7:23)

Mifano ya taabu ya madeni

Daudi akaondoka Gathi na kukimbilia kwenye pango la Adulamu. Ndugu zake na watu wa nyumba ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. Wale wote waliokuwa katika dhiki au waliokuwa na madeni au wale ambao hawakuridhika wakamkusanyikia Daudi, naye akawa kiongozi wao. Watu wapatao 400 walikuwa pamoja naye. (1 Samweli 22:1-2)
Mke wa mmoja wa wana wa manabii akamlilia Elisha, akamwambia, “Mtumishi wako, mume wangu, amekufa, nawe unajua alikuwa anamcha Bwana. Lakini sasa yule anayemdai anakuja kuchukua wanangu wawili kama watumwa wake.” (2 Wafalme 4:1)
Wakati huu wanaume na wake zao wakalia kilio kikuu dhidi ya ndugu zao Wayahudi. Baadhi yao walikuwa wakisema, “Sisi na wana wetu na binti zetu tuko wengi. Ili tuweze kula na kuishi, ni lazima tupate nafaka.” Wengine walikuwa wakisema, “Tunaweka rehani mashamba yetu, mashamba ya mizabibu, na nyumba zetu ili tupate nafaka wakati wa njaa.” Bado kukawa na wengine waliokuwa wakisema, “Ilitubidi tukope fedha ili kulipa kodi ya mfalme kwa ajili ya mashamba yetu na mashamba yetu ya mizabibu. Ingawa sisi ni mwili na damu moja sawa na watu wa nchi yetu, na ijapo wana wetu ni wazuri kama wana wao, bado inatupasa kuwatoa wana wetu na binti zetu kwenye utumwa. Baadhi ya binti zetu wameshakuwa watumwa tayari, lakini hatuna uwezo wa kuwakomboa, kwa sababu mashamba yetu na mashamba ya mizabibu yetu ni mali ya wengine.” (Nehemia 5:1-5)
Mtu anayemdai na ateke vyote alivyo navyo, matunda ya kazi yake yatekwe nyara na wageni. (Zaburi 109:11)
Hili ndilo asemalo Bwana: “Iko wapi hati ya talaka ya mama yako ambayo kwayo niliachana naye? Au nimewauza ninyi kwa nani miongoni mwa watu wanaonidai? Kwa ajili ya dhambi zenu mliuzwa, kwa sababu ya makosa, mama yenu aliachwa. (Isaya 50:1)

Kutokuwa na deni kulikuwa jambo jema

Ole wangu, mama yangu, kwamba ulinizaa, mtu ambaye ulimwengu wote unashindana na kugombana naye! Sikukopa wala sikukopesha, lakini kila mmoja ananilaani. (Yeremia 15:10)

Deni lilionekana kama laana

Hata hivyo, kama hutamtii Bwana Mungu wako na kuzishika kwa bidii amri zake zote na maagizo ninayokupa leo, laana hizi zote zitakuja juu yako na kukupata: Mgeni anayeishi miongoni mwako atainuka juu zaidi na zaidi kuliko wewe, lakini wewe utashuka chini zaidi na zaidi. Yeye atakukopesha, lakini wewe hutamkopesha. Yeye atakuwa kichwa, lakini wewe utakuwa mkia. Laana hizi zote zitakuja juu yako. Zitakufuatia na kukupata mpaka uangamizwe, kwa sababu hukumtii Bwana Mungu wako, na kuzishika amri zake na maagizo yake aliyokupa. (Kumbukumbu 28:15, 43-45)

Kutokuwa na deni kulionekana kama baraka

Hata hivyo, hapatakuwepo maskini miongoni mwenu, kwa kuwa katika nchi Bwana Mungu wenu anayowapa kuimiliki kama urithi wenu, atawabariki sana, ikiwa tutamtii Bwana Mungu wenu kikamilifu na kuwa waangalifu kuyafuata maagizo haya yote ninayowapa leo. Kwa kuwa Bwana Mungu wenu atawabariki kama alivyoahidi, nanyi mtawakopesha mataifa mengi lakini hamtakopa kwa yeyote. Mtatawala mataifa mengi lakini hakuna taifa litakalowatawala ninyi. (Kumbukumbu 15:4-6)
Kama ukimtii Bwana Mungu wako kwa bidii na kufuata amri zake zote ninazokupa leo kwa bidii, Bwana Mungu wako atakuweka juu ya mataifa yote katika dunia. Baraka hizi zote zitakuja juu yako na kukupata, kama ukimtii Bwana Mungu wako: Bwana atafungua mbingu, ghala zake za baraka, kukupa mvua kwa majira yake na kubariki kazi zako zote za mikono yako. Utakopesha mataifa mengi lakini hutakopa kwa yeyote. (Kumbukumbu 28:1-2, 12)

Kulipa madeni

Watu wanaomcha Mungu hulipa madeni yao

Usizuie wema kwa wale wanaostahili ikiwa katika uwezo wako kutenda. Usimwambie jirani yako, “Njoo baadaye, nitakupa kesho”: wakati wewe unacho kitu kile karibu nawe. (Mithali 3:27-28)

Waovu hawalipi madeni yao

Waovu hukopa na hawalipi, bali wenye haki hutoa kwa ukarimu. (Zaburi 37:21)

Bwana anaweza kwa njia ya muujiza kutoa rasilimali za kutoka katika madeni

Mke wa mmoja wa wana wa manabii akamlilia Elisha, akamwambia, “Mtumishi wako, mume wangu, amekufa, nawe unajua alikuwa anamcha Bwana. Lakini sasa yule anayemdai anakuja kuchukua wanangu wawili kama watumwa wake.” Elisha akamjibu, “Nitawezaje kukusaidia? Niambie, una nini ndani ya nyumba yako?” Akasema, “Mtumishi wako hana kitu chochote kabisa, isipokuwa mafuta kidogo.” Elisha akasema, “Zunguka kwa majirani zako wote ukaombe vyombo vitupu. Usiombe vichache. Kisha ingia ndani na ujifungie mlango, wewe na wanao. Mimina mafuta kwenye vyombo vyote, na kila kimoja kinapojaa, kiweke kando.” Yule mjane akaondoka na kujifungia ndani, yeye na wanawe. Wao wakamletea vyombo, naye akaendelea kumimina mafuta. Vyombo vyote vilipojaa, akamwambia mwanawe, “Niletee chombo kingine.” Lakini mwanawe akajibu, “Hakuna chombo kingine kilichobaki.” Basi mafuta yakakoma kutiririka. Yule mwanamke akaenda akamwambia yule mtu wa Mungu, naye mtu wa Mungu akasema, “Nenda ukayauze hayo mafuta ulipe madeni yako. Wewe na wanao mnaweza kuishi kwa kile kinachosalia.” (2 Wafalme 4:1-7)

Kusamehe madeni kila mwaka wa saba – sheria kwa waamini wa Agano la Kale

Kila mwisho wa miaka saba ni lazima mfute madeni. Hivi ndivyo itakavyofanyika: Kila mkopeshaji atafuta mkopo aliomkopesha Mwisraeli mwenzake. Hatamtaka Mwisraeli mwenzake au ndugu yake amlipe hilo deni, kwa sababu wakati wa Bwana wa kufuta madeni umetangazwa. Unaweza kudai malipo kwa mgeni, lakini lazima ufute kila deni ambalo unamdai ndugu yako. Hata hivyo, hapatakuwepo maskini miongoni mwenu, kwa kuwa katika nchi Bwana Mungu wenu anayowapa kuimiliki kama urithi wenu, atawabariki sana, ikiwa tutamtii Bwana Mungu wenu kikamilifu na kuwa waangalifu kuyafuata maagizo haya yote ninayowapa leo. Kwa kuwa Bwana Mungu wenu atawabariki kama alivyoahidi, nanyi mtawakopesha mataifa mengi lakini hamtakopa kwa yeyote. Mtatawala mataifa mengi lakini hakuna taifa litakalowatawala ninyi. Ikiwa kuna mtu maskini miongoni mwa ndugu zenu, katika mji wowote wa hiyo nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa, msiwe na moyo mgumu wala usimfumbie mkono ndugu yako aliye maskini. Afadhali fungua mikono yako na umkopeshe kwa hiari chochote anachohitaji. Jihadhari usijiwekee wazo hili ovu: “Mwaka wa saba, mwaka wa kufuta madeni umekaribia,” usije ukaonyesha nia mbaya kwa ndugu yako mhitaji na ukaacha kumpa chochote. Anaweza kumlalamikia Bwana dhidi yako nawe utakuwa umepatikana na hatia ya dhambi. Mpe kwa ukarimu na ufanye hivyo bila kinyongo moyoni, ndipo kwa sababu ya hili Bwana Mungu wenu atakubariki katika kazi zako zote na kwa kila kitu utakachokiwekea mkono wako. Siku zote watakuwepo watu maskini katika nchi. Kwa hiyo ninawaamuru mwe na mikono iliyokunjuliwa kuwaelekea ndugu zenu, kuwaelekea maskini na wahitaji katika nchi yenu. (Kumbukumbu 15:1-11)
Kisha Mose akawaamuru, akasema: “Mwishoni mwa kila miaka saba, katika mwaka wa kufuta madeni, wakati wa Sikukuu ya Vibanda, Waisraeli wote wanapokuja mbele za Bwana Mungu wenu mahali atakapopachagua, utasoma sheria hii mbele yao masikioni mwao. (Kumbukumbu 31:10-11)
“Wakati mataifa jirani waletapo bidhaa zao au nafaka kuuza siku ya Sabato, hatutazinunua kutoka kwao siku ya Sabato, wala siku nyingine yoyote takatifu. Kila mwaka wa saba, tutaacha kuilima ardhi na tutafuta madeni yote. (Nehemia 10:31)

Mfano mwingine wa kulipa deni

Kama amekukosea lolote au kama unamdai chochote, nidai mimi. Ni mimi Paulo, ninayeandika waraka huu kwa mkono wangu mwenyewe. Nitakulipa. Sitaji kwamba nakudai hata nafsi yako. (Filemoni 18-19)

Madeni yametumika kama mifano katika mafundisho

Mafundisho ya Yesu Kristo

Ndipo Petro akamjia Yesu na kumuuliza, “Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Je, hata mara saba?” Yesu akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. “Kwa hiyo Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme aliyetaka kufanya hesabu zake za fedha na watumishi wake. Alipoanza kufanya hesabu zake, mtu mmoja aliyekuwa anadaiwa talanta 10,000, aliletwa kwake. Kwa kuwa alikuwa hawezi kulipa deni hilo, bwana wake akaamuru kwamba auzwe, yeye, mkewe, watoto wake na vyote alivyokuwa navyo, ili lile deni lipate kulipwa. “Yule mtumishi akampigia magoti, akamsihi yule bwana akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’ Yule bwana wa huyo mtumishi akamwonea huruma, akafuta deni lake lote, akamwacha aende zake. “Lakini yule mtumishi alipokuwa anatoka nje, akakutana na mtumishi mwenzake aliyekuwa amemkopesha dinari mia moja. Akamkamata, akamkaba koo akimwambia, ‘Nilipe kile ninachokudai!’ “Yule mtumishi mwenzake akapiga magoti akamsihi akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’ “Lakini akakataa. Badala yake, alienda akamtupa gerezani hata atakapolipa hilo deni. Watumishi wenzake walipoona haya yaliyotukia wakaudhika sana, nao wakaenda na kumwambia bwana wao kila kitu kilichokuwa kimetukia. “Yule bwana akamwita yule mtumishi akamwambia, ‘Wewe mtumishi mwovu! Mimi nilikusamehe deni lako lote uliponisihi. Je, haikukupasa kumhurumia mtumishi mwenzako kama mimi nilivyokuhurumia wewe?’ Kwa hasira, yule bwana wake akamtia yule mtumishi mikononi mwa askari wa gereza ili ateswe mpaka atakapolipa yote aliyokuwa anadaiwa. “Hivi ndivyo Baba yangu wa mbinguni atakavyomfanyia kila mmoja wenu ikiwa hatamsamehe ndugu yake kutoka moyoni mwake.” (Mathayo 18:21-35)
Yesu akanena akamwambia, “Simoni, nina jambo la kukuambia.” Simoni akajibu, “Mwalimu, sema.” “Palikuwa na mtu mmoja aliyewakopesha watu wawili fedha: Mmoja alidaiwa dinari 500 na mwingine dinari hamsini. Wote wawili walipokuwa hawawezi kulipa, aliyafuta madeni yao wote wawili. Sasa ni yupi kati yao atakayempenda yule aliyewasamehe zaidi?” Simoni akajibu, “Nadhani ni yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi.” Naye Yesu akamwambia, “Umehukumu kwa usahihi.” (Luka 7:40-43)

Mafundisho ya Paulo

...akiisha kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili, pamoja na maagizo yake. Aliiondoa isiwepo tena, akiigongomea kwenye msalaba wake. (Wakolosai 2:14)

Kuwa mdhamini wa deni la mwingine (dhamana/kupeana mikono)

Kuwa mdhamini hakuhimizwi

Mtu mjinga hupana mkono ili kuweka rehani, naye huweka dhamana kwa jirani yake. (Mithali 17:18)
Chukua vazi la yule awekaye dhamana kwa ajili ya mgeni; lishikilie iwe dhamana kama anafanya hivyo kwa ajili ya mwanamke mpotovu. (Mithali 20:16)
Chukua vazi la yule awekaye dhamana kwa ajili ya mgeni; lishikilie iwe dhamana kama anafanya hivyo kwa ajili ya mwanamke mpotovu. (Mithali 27:13)

Kuwa mdhamini ni hatari

Yeye amdhaminiye mgeni hakika atateseka, bali yeyote akataaye kuunga mkono dhamana ni salama. (Mithali 11:15)
Usiwe mwenye kupana mikono katika rehani, au kuweka dhamana kwa ajili ya madeni. Kama ukikosa njia ya kulipa, kitanda chako kitachukuliwa ukiwa umekilalia. (Mithali 22:26-27)

Kuokolewa kutoka katika udhamini

Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa jirani yako, ikiwa umeshika mikono kwa kuweka ahadi kwa ajili ya mwingine, kama umetegwa na ulichosema, umenaswa kwa maneno ya kinywa chako, basi fanya hivi mwanangu, ili ujiweke huru, kwa kuwa umeanguka mikononi mwa jirani yako: Nenda ukajinyenyekeshe kwake; msihi jirani yako! Usiruhusu usingizi machoni pako, usiruhusu kope zako zisinzie. Jiweke huru, kama swala mkononi mwa mwindaji, kama ndege kutoka kwenye mtego wa mwindaji. (Mithali 6:1-5)