Mengineyo

Vifungu hivi vinazungumzia vipengele mbalimbali vya biashara, fedha na asili ya mwanadamu, vikionyesha hatari za choyo, udanganyifu na vipaumbele visivyo sahihi. Vinasisitiza umuhimu wa uadilifu, kuridhika na kumtegemea Mungu katika kila nyanja ya maisha, ikiwemo biashara.

Biashara

Waliagiza magari kutoka Misri kwa bei ya shekeli 600 za fedha na farasi kwa shekeli 150. Pia waliwauza nje kwa wafalme wote wa Wahiti na wa Waaramu. (1 Wafalme 10:29)
“Haifai, haifai!” asema mnunuzi, kisha huondoka akijisifia ununuzi wake. (Mithali 20:14)
Basi sikilizeni ninyi msemao, “Leo au kesho tutakwenda katika mji huu ama ule tukae humo mwaka mmoja, tufanye biashara na kupata faida.” Lakini hamjui hata litakalotukia kesho. Maisha yenu ni nini? Ninyi ni ukungu ambao huonekana kwa kitambo kidogo kisha hutoweka. Badala yake, inawapasa kusema, “Kama Bwana akipenda, tutaishi na kufanya hili ama lile.” (Yakobo 4:13-15)

Matokeo ya kifedha ya uzinzi

...wageni wasije wakasherehekea utajiri wako na jitihada yako ikatajirisha nyumba ya mwanaume mwingine. (Mithali 5:10)
Hatakubali fidia yoyote; atakataa malipo, hata yakiwa makubwa kiasi gani. (Mithali 6:35)
Mtu apendaye hekima huleta furaha kwa baba yake, bali aambatanaye na makahaba hutapanya mali yake. (Mithali 29:3)

Moyo wa mwanadamu

Usile chakula cha mtu mchoyo, usitamani vyakula vyake vitamu, kwa maana yeye ni aina ya mtu ambaye kila mara anafikiri juu ya gharama. Anakuambia, “Kula na kunywa,” lakini moyo wake hauko pamoja nawe. Utatapika kile kidogo ulichokula, nawe utakuwa umepoteza bure maneno yako ya kumsifu. (Mithali 23:6-8)
Watu wangu wanakujia, kama wafanyavyo, nao wanaketi mbele yako kama watu wangu na kusikiliza maneno yako, lakini hawayatendi. Kwa maana udanganyifu u katika midomo yao, lakini mioyo yao ina tamaa ya faida isiyo halali. (Ezekieli 33:31)
Lakini ikiwa mna wivu na ni wenye chuki na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu kwa ajili ya hayo wala msiikatae kweli. Hekima ya namna hiyo haishuki kutoka mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyo ya kiroho, na ya kishetani. Kwa maana panapokuwa na wivu na ubinafsi, ndipo penye machafuko na uovu wa kila namna. (Yakobo 3:14-16)
Mnatamani lakini hampati, kwa hiyo mwaua. Mwatamani kupata lakini hampati vile mnavyotaka, kwa hiyo mnajitia katika magomvi na mapigano. Mmepungukiwa kwa sababu hammwombi Mungu. Mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya, ili mpate kuvitumia hivyo mtakavyopata kwa tamaa zenu. (Yakobo 4:2-3)
Nao katika tamaa zao mbaya, walimu hawa watajipatia faida kwenu kwa hadithi walizotunga wenyewe. Lakini hukumu imekwisha kutangazwa dhidi yao tangu zamani, wala uangamivu wao haujalala usingizi. (2 Petro 2:3)

Sheria ya Agano la Kale kuhusu ndoa

Lakini kama hutaendelea kupendezwa naye, mwache aende popote anapotaka. Kamwe huwezi kumuuza au kumtendea kama mtumwa, kwa sababu utakuwa umemvunjia heshima. (Kumbukumbu 21:14)

Wengine hawajali fedha

Tazama, nitawachochea Wamedi dhidi yao, ambao hawajali fedha wala hawafurahii dhahabu. (Isaya 13:17)
Wagibeoni wakamjibu, “Hatuna haki ya kudai fedha wala dhahabu kutoka kwa Sauli au jamaa yake, wala hatuna haki ya kumuua mtu yeyote katika Israeli.” Daudi akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?” (2 Samweli 21:4)

Mengineyo

Akamwambia, “Binti yangu, ubarikiwe na Bwana. Wema huu wa sasa ni mkuu kushinda hata ule ulioonyesha mwanzoni. Hukuwakimbilia vijana, wakiwa matajiri au maskini. (Ruthu 3:10)
Watu humlaani mtu awanyimae watu nafaka, bali baraka itamkalia kichwani kama taji yeye aliye radhi kuiuza. (Mithali 11:26)
Heri mtu wa hali ya chini mwenye mtumishi, kuliko kujifanya mtu wa hali ya juu nawe huna chakula. (Mithali 12:9)
Nunua kweli wala usiiuze, pata hekima, adabu na ufahamu. (Mithali 23:23)
Wakamfanyia kaburi pamoja na waovu, pamoja na matajiri katika kifo chake, ingawa hakutenda jeuri, wala hapakuwa na hila kinywani mwake. (Isaya 53:9)
Akawaambia, “Basi kila mwalimu wa sheria aliyefundishwa elimu ya Ufalme wa Mbinguni ni kama mwenye nyumba anayetoa kutoka ghala yake mali mpya na mali ya zamani.” (Mathayo 13:52)
Hapo palikuwa na mwanamke aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili. Mwanamke huyu alikuwa ameteseka sana kwa mikono ya matabibu wengi, na kutumia kila kitu alichokuwa nacho. Lakini badala ya kupona, hali yake ilizidi kuwa mbaya. (Marko 5:25-26)
Ndipo yule jemadari akasema, “Mimi ilinigharimu kiasi kikubwa cha fedha kupata uraia wangu.” Paulo akasema “Lakini mimi ni raiya wa Rumi kwa kuzaliwa.” (Matendo 22:28)

Usimtoze mwenye haki faini

Si vizuri kumwadhibu mtu asiye na hatia, au kuwapiga sana maafisa kwa ajili ya uadilifu wao. (Mithali 17:26)

Hukumu za Bwana

Katika siku ile, kila mahali palipokuwa na mizabibu elfu moja yenye thamani ya shekeli 1,000 za fedha, patakuwa na michongoma na miiba tu. (Isaya 7:23)
Lakini faida na mapato yake yatawekwa wakfu kwa Bwana; hayatahifadhiwa wala kufichwa. Faida zake zitakwenda kwa wale wakaao mbele za Bwana kwa ajili ya chakula tele na mavazi mazuri. (Isaya 23:18)

Masiya atafanikiwa

Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa hekima; atatukuzwa, na kuinuliwa juu, na kukwezwa sana. (Isaya 52:13)
Lakini yalikuwa ni mapenzi ya Bwana kumchubua na kumsababisha ateseke. Ingawa Bwana amefanya maisha yake kuwa sadaka ya hatia, ataona uzao wake na kuishi siku nyingi, nayo mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake. (Isaya 53:10)

Uhusiano na Bwana hauwezi kununuliwa

“Njooni, ninyi nyote wenye kiu, njooni kwenye maji; nanyi ambao hamna fedha, njooni, nunueni na mle! Njooni, nunueni divai na maziwa bila fedha na bila gharama. Kwa nini kutumia fedha kwa kitu ambacho si chakula, na kutaabikia kitu kisichoshibisha? Sikilizeni, nisikilizeni mimi na mle kilicho kizuri, nazo nafsi zenu zitafurahia utajiri wa unono. (Isaya 55:1-2)

Kutokuwa mwaminifu kunalinganishwa na ukahaba

Kila kahaba hupokea malipo, lakini wewe hutoa zawadi kwa wapenzi wako wote, ukiwahonga ili waje kwako kutoka kila mahali kwa ajili ya ukahaba wako. Kwa hiyo wewe ulikuwa tofauti na wanawake wengine kwenye ukahaba wako, hakuna aliyekutongoza ili kuzini naye, wewe ndiye uliyelipa wakati hakuna malipo uliyolipwa wewe. Wewe ulikuwa tofauti. (Ezekieli 16:33-34)

Sheria kuhusu makuhani na ardhi

Hawataruhusiwa kuuza wala kuibadilisha hata mojawapo. Hii ndiyo sehemu nzuri ya nchi kuliko nyingine zote, hivyo haitakuwa mikononi mwa watu wengine, kwa sababu ni takatifu kwa Bwana. (Ezekieli 48:14)

Wasiomcha Mungu humthamini Bwana kidogo

Nikawaambia, “Mkiona kuwa ni vyema, nipeni ujira wangu, la sivyo, basi msinipe.” Kwa hiyo wakanilipa vipande thelathini vya fedha. Naye Bwana akaniambia, “Mtupie mfinyanzi,” hiyo bei nzuri waliyonithaminia! Kwa hiyo nikachukua hivyo vipande thelathini vya fedha na kumtupia huyo mfinyanzi katika nyumba ya Bwana. (Zekaria 11:12-13)

Aliye na kitu ataongezewa; asiye na kitu atanyang'anywa vyote

Naye akawaambia, “Kuweni waangalifu na yale mnayosikia. Kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa ninyi, hata na zaidi. Kwa maana kila mtu aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyangʼanywa.” (Marko 4:24-25)

Fedha zimetumika kuonyesha furaha ya malaika kwa ajili ya wokovu

“Au ikiwa mwanamke ana sarafu za fedha kumi, naye akapoteza moja, je, hawashi taa na kufagia nyumba na kuitafuta kwa bidii mpaka aipate? Naye akiisha kuipata, huwaita rafiki zake na majirani na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami; nimeipata ile sarafu yangu ya fedha iliyopotea.’ Vivyo hivyo, nawaambia, kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu juu ya mwenye dhambi mmoja atubuye.” (Luka 15:8-10)

Mtazamo juu ya umiliki katika kanisa la kwanza

Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake. (Matendo 2:44-45)
Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. Wala hapakuwepo mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake. Yosefu, Mlawi kutoka Kipro, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake Mwana wa Faraja), aliuza shamba alilokuwa nalo, akaleta hizo fedha alizopata na kuziweka miguuni pa mitume. (Matendo 4:32-37)

Wanaomjua Bwana huacha mambo maovu ya gharama kubwa

Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu. Idadi kubwa ya wale waliofanya mambo ya uganga wakaleta vitabu vyao na kuviteketeza kwa moto hadharani. Walipofanya hesabu ya thamani ya vitabu vilivyoteketezwa ilikuwa drakma 50,000 za fedha. (Matendo 19:18-19)

Kuthibitishwa haki

Akamwambia Sara, “Ninampa kaka yako shekeli elfu moja za fedha. Hii ni kufidia kosa lililofanyika dhidi yako mbele ya wote walio pamoja nawe; haki yako imethibitishwa kabisa.” (Mwanzo 20:16)

Nyara, mateka

Wana wa Yakobo walipita juu ya maiti katika kuteka nyara mji ule ambamo dada yao alikuwa amenajisiwa. Wakachukua kondoo na mbuzi, ngʼombe, punda na kila kitu kilichokuwa chao ndani ya mji ule na mashambani. Walichukua utajiri wao wote pamoja na wanawake na watoto wao, wakachukua nyara kila kitu ndani ya nyumba zao. (Mwanzo 34:27-29)
Waisraeli waliporudi kutoka kuwafukuza Wafilisti, waliteka nyara kutoka kambi yao. (1 Samweli 17:53)
Wakati huu, Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akakusanya jeshi lake lote. Akifuatana na wafalme thelathini na wawili wakiwa na farasi na magari ya vita, akakwea kuuzingira kwa jeshi Samaria na kuishambulia. Akawatuma wajumbe katika mji kwa Ahabu mfalme wa Israeli, kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi: ‘Fedha yako na dhahabu ni yangu, nao wake zako walio wazuri sana na watoto ni wangu.’ ” Mfalme wa Israeli akajibu, “Iwe kama usemavyo, bwana wangu mfalme. Mimi na vyote nilivyo navyo ni mali yako.” Wale wajumbe wakaja tena na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi: ‘Nimetuma kutaka fedha yako na dhahabu, wake zako na watoto wako. Lakini kesho wakati kama huu, nitawatuma maafisa wangu kukagua jumba lako la kifalme na nyumba za maafisa wako. Watatwaa kitu unachokithamini nao watakichukua.’ ” Wazee na watu wote wakajibu, “Usimsikilize, wala usiyakubali matakwa yake.” (1 Wafalme 20:1-6, 8)
Yuda ikashindwa na Israeli, na kila mtu akakimbilia nyumbani kwake. Akachukua dhahabu yote na fedha na vyombo vyote vilivyopatikana ndani ya Hekalu la Bwana na katika hazina zote za jumba la mfalme. Akachukua pia mateka na akarudi Samaria. (2 Wafalme 14:12, 14)
Hivyo Yehoshafati na watu wake wakaenda kujitwalia nyara kutoka kwao, nao wakakuta humo wingi wa mifugo, mali, nguo na vitu vya thamani, ambavyo vilikuwa vingi zaidi ya vile walivyoweza kuchukua. Wakakusanya nyara kwa siku tatu kwa sababu zilikuwa nyingi mno. (2 Nyakati 20:25)
Tokea siku za babu zetu mpaka sasa, hatia yetu imekuwa kubwa. Kwa sababu ya dhambi zetu, sisi na wafalme wetu na makuhani wetu tumekabiliwa na vita, utumwa, kutekwa na kudhiliwa katika mikono ya wafalme wa kigeni, kama ilivyo leo. (Ezra 9:7)
Waraka wa mfalme uliwaruhusu Wayahudi katika kila mji kuwa na haki ya kukusanyika na kujilinda wenyewe; kuharibu, kuua na kuangamiza jeshi lolote, taifa lolote au jimbo lile litakalowashambulia wao, wake zao, watoto wao na kuteka mali za adui zao. (Esta 8:11)
Wayahudi waliwaangusha adui zao wote kwa upanga wakiwaua na kuwaangamiza, nao walifanya kile walichotaka kwa wale waliowachukia. wana kumi wa Hamani mwana wa Hamedatha, adui wa Wayahudi. Lakini hawakuchukua nyara. (Esta 9:5, 10)
“Ole kwa Ashuru, fimbo ya hasira yangu, ambaye mkononi mwake ana rungu ya ghadhabu yangu! Ninamtuma dhidi ya taifa lisilomjua Mungu, ninamtuma dhidi ya taifa linalonikasirisha, kukamata mateka na kunyakua nyara, pia kuwakanyaga chini kama matope ya barabarani. (Isaya 10:5-6)
Bwana atakapokuwa amemaliza kazi yake yote dhidi ya Mlima Sayuni na Yerusalemu, atasema, “Nitamwadhibu mfalme wa Ashuru kwa ajili ya majivuno ya ukaidi wa moyo wake na kutazama kwa macho yenye dharau.” Kwa kuwa anasema: “ ‘Kwa nguvu za mkono wangu nimefanya hili, kwa hekima yangu, kwa sababu nina ufahamu. Niliondoa mipaka ya mataifa, niliteka nyara hazina zao, kama yeye aliye shujaa niliwatiisha wafalme wao. Kama mtu atiavyo mkono kwenye kiota, ndivyo mkono wangu ulivyochukua utajiri wa mataifa; kama watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya nchi zote; wala hakuna hata mmoja aliyepiga bawa au kufungua kinywa chake kutoa mlio.’ ” (Isaya 10:12-14)
Watateka utajiri wako na kuchukua nyara bidhaa zako, watazivunja kuta zako na kuzibomoa nyumba zako nzuri, watatupa baharini mawe yako, mbao zako na kifusi chako. (Ezekieli 26:12)
Upanga utakuja dhidi ya Misri, nayo maumivu makuu yataijia Ethiopia. Mauaji yatakapoangukia Misri, utajiri wake utachukuliwa na misingi yake itabomolewa. (Ezekieli 30:4)
...hata ingawa Efraimu atastawi miongoni mwa ndugu zake. Upepo wa mashariki kutoka kwa Bwana utakuja, ukivuma kutoka jangwani, chemchemi yake haitatoa maji na kisima chake kitakauka. Ghala lake litatekwa hazina zake zote. (Hosea 13:15)
Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: “Adui ataizingira nchi; ataangusha chini ngome zenu na kuteka nyara maboma yenu.” (Amosi 3:11)
Usingeingia katika malango ya watu wangu katika siku ya maafa yao, wala kuwadharau katika janga lao katika siku ya maafa yao, wala kunyangʼanya mali zao katika siku ya maafa yao. (Obadia 1:13)
Lakini tazama jinsi Esau atakavyotekwa, jinsi hazina zake zilizofichwa zitatekwa nyara! Siku ile ulisimama mbali ukiangalia wakati wageni walipojichukulia utajiri wake na watu wa nchi nyingine walipoingia malango yake wakipiga kura kwa ajili ya Yerusalemu, ulikuwa kama mmoja wao. (Obadia 1:6, 11)
“Inuka upure, ee Binti Sayuni, kwa kuwa nitakupa pembe za chuma; nitakupa kwato za shaba na utavunja vipande vipande mataifa mengi.” Utatoa mapato yao waliopata kwa udanganyifu kwa Bwana, utajiri wao kwa Bwana wa dunia yote. (Mika 4:13)
Chukueni nyara za fedha! Chukueni nyara za dhahabu! Wingi wake hauna mwisho, utajiri kutoka hazina zake zote! Ameharibiwa, ametekwa nyara, ameachwa uchi! Mioyo inayeyuka, magoti yanalegea, miili inatetemeka, na kila uso umebadilika rangi. (Nahumu 2:9-10)
Ole wa mji umwagao damu, uliojaa uongo, umejaa nyara, usiokosa kuwa na vitu vya kuteka nyara. (Nahumu 3:1)
“Je, watu wote hawatamsuta kwa dhihaka na kumbeza, wakisema, “ ‘Ole wake yeye akusanyaye bidhaa zilizoibwa na kujifanyia utajiri kwa kutoza kwa nguvu! Ataendelea hivi kwa muda gani?’ Je, wadai wako hawatainuka ghafula? Je, hawataamka na kukufanya utetemeke? Kisha utakuwa mhanga kwao. Kwa kuwa umeteka nyara mataifa mengi, watu waliobaki watakuteka nyara wewe. Kwa kuwa umemwaga damu ya mtu; umeharibu nchi na miji, na kila mmoja ndani yake. (Habakuki 2:6-8)
Ombolezeni, ninyi mnaoishi katika eneo la sokoni; wafanyabiashara wenu wote wameangamizwa, wote ambao wanafanya biashara ya fedha wataangamizwa. Utajiri wao utatekwa nyara, nyumba zao zitabomolewa. Watajenga nyumba, lakini hawataishi ndani yake; watapanda mizabibu lakini hawatakunywa divai yake. Fedha yao wala dhahabu yao hazitaweza kuwaokoa katika siku hiyo ya ghadhabu ya Bwana. Katika moto wa wivu wake dunia yote itateketezwa, kwa maana ataleta mwisho wa wote wanaoishi katika dunia ghafula.” (Sefania 1:11, 13, 18)
Hakika, kama niishivyo,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, “hakika Moabu itakuwa kama Sodoma, Waamoni kama Gomora: mahali pa magugu na mashimo ya chumvi, nchi ya ukiwa milele. Mabaki ya watu wangu watawateka nyara; mabaki ya taifa langu watarithi nchi yao.” (Sefania 2:9)

Mtindo wa maisha

Nia yetu si kwamba wengine wasaidike wakati ninyi mnateseka, bali pawe na uwiano. Kwa wakati huu, wingi wa vitu mlivyo navyo usaidie kutosheleza mahitaji yao, ili wakati wao watakapokuwa na wingi wa vitu, nao wapate kutosheleza mahitaji yenu. Ndipo patakuwa na usawa, kama ilivyoandikwa: “Aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa.” (2 Wakorintho 8:13-15)
Vivyo hivyo nataka wanawake wajipambe kwa adabu na kwa heshima katika mavazi yanayostahili, si kwa kusuka nywele, kuvalia dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa, (1 Timotheo 2:9)

Kurudisha kilichoharibiwa

“Kama watu wakigombana na mmoja akimpiga mwingine kwa jiwe au kwa ngumi yake na hakufa bali akaugua na kulala kitandani, yule aliyempiga ngumi hatahesabiwa kuwa na hatia kama mwenzake ataamka na kujikongoja kwa fimbo yake, lakini hata hivyo, ni lazima amlipe fidia ya muda wake aliopoteza na awajibike mpaka apone kabisa. (Kutoka 21:18-19)
“Ikiwa watu wawili wanapigana na wakamuumiza mwanamke mjamzito, naye akazaa kabla ya wakati lakini hakuna majeraha makubwa, mhalifu atatozwa mali kiasi cha madai ya mume wa yule mwanamke, na jinsi mahakama itakavyoamua. (Kutoka 21:22)
“Kama fahali akimuua mwanaume au mwanamke kwa kumpiga kwa pembe, fahali huyo ni lazima auawe kwa kupigwa mawe, na nyama yake haitaliwa. Lakini mwenye fahali huyo hatawajibika. Lakini hata hivyo, ikiwa huyo fahali amekuwa na tabia ya kupiga kwa pembe, na mwenyewe ameonywa na hakutaka kumfungia naye akamuua mwanaume au mwanamke, huyo fahali ni lazima auawe kwa mawe na mwenye fahali pia auawe. Lakini ikiwa malipo yatatakiwa kwake, basi anaweza kulipa kinachodaiwa ili kuukomboa uhai wake. (Kutoka 21:28-30)
Ikiwa fahali atampiga mtumwa wa kike au wa kiume, mwenye fahali atalipa shekeli thelathini za fedha kwa bwana mwenye mtumwa, na fahali ni lazima auawe kwa mawe. “Kama mtu akiacha shimo wazi, ama akachimba shimo kisha asilifukie, na ngʼombe au punda akatumbukia ndani yake, mwenye shimo ni lazima alipe hasara iliyotokea; ni lazima amlipe mwenye mnyama. Mnyama aliyekufa atakuwa wake. “Kama fahali wa mtu fulani atamuumiza fahali wa mtu mwingine na akafa, watamuuza yule aliye hai na wagawane sawa fedha pamoja na mnyama aliyekufa. Hata hivyo, kama ikifahamika kwamba fahali huyo alikuwa na tabia ya kupiga kwa pembe na mwenyewe hakumfunga, ni lazima mwenye fahali alipe mnyama kwa mnyama, na mnyama aliyekufa atakuwa wake. (Kutoka 21:32-36)

Viongozi

Samweli akawaambia wale watu waliokuwa wakiomba wapewe mfalme maneno yote ya Bwana. Akasema, “Hivi ndivyo atakavyowatendea mfalme atakayewatawala. Atawachukua wana wenu na kuwafanya watumike kwa magari yake ya vita na farasi, nao watakimbia mbele ya magari yake. Atayachukua mashamba yenu yaliyo mazuri, mashamba ya mizabibu na mashamba yenu ya mizeituni na kuwapa watumishi wake. Ataichukua sehemu ya kumi ya nafaka yenu na ya zabibu zenu na kuwapa maafisa wake na watumishi wake. Atawachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike, na ngʼombe wenu walio wazuri sana na punda kwa matumizi yake mwenyewe. Atachukua sehemu ya kumi ya makundi yenu ya kondoo na mbuzi, na ninyi wenyewe mtakuwa watumwa wake. (1 Samweli 8:10-11, 14-17)
“ ‘Mkuu anayetawala atakuwa na lile eneo linalopakana na lile eneo lililowekwa wakfu upande huu na upande huu na eneo la mji. Eneo la mji litaenea upande wa magharibi kuanzia upande wa magharibi na upande wa mashariki kuanzia upande wa mashariki, likiendelea kwa urefu kutoka magharibi hadi mpaka wa mashariki sambamba na mojawapo ya sehemu za makabila. Nchi hii itakuwa milki yake katika Israeli. Nao wakuu wangu hawataonea tena watu wangu bali watairuhusu nyumba ya Israeli kuimiliki nchi kulingana na makabila yao. (Ezekieli 45:7-8)

Unabii

Yeremia akasema, “Neno la Bwana lilinijia kusema: Hanameli mwana wa Shalumu mjomba wako atakuja kwako na kusema, ‘Nunua shamba langu huko Anathothi, kwa sababu wewe kama jamaa ya karibu ni haki na wajibu wako kulinunua.’ Hivyo nikalinunua shamba hilo lililoko Anathothi kutoka kwa binamu yangu Hanameli, nami nikampimia shekeli kumi na saba za fedha. ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Chukua hati hizi, yaani nakala zote zenye muhuri na zisizo na muhuri za hati ya kununulia, na uziweke kwenye gudulia la udongo wa mfinyanzi ili zidumu kwa muda mrefu. Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Nyumba, mashamba na mashamba ya mizabibu yatanunuliwa tena katika nchi hii.’ (Yeremia 32:6-7, 9, 14-15)
Ingawa mji utatiwa mikononi mwa Wakaldayo, wewe, Ee Bwana Mwenyezi, uliniambia, ‘Nunua shamba kwa fedha, na jambo hilo lishuhudiwe.’ ” (Yeremia 32:25)
Jeuri imeinuka kuwa fimbo ya kuadhibu uovu, hakuna hata mmoja wa hao watu atakayeachwa, hata mmoja wa kundi lile, hakuna utajiri, hakuna chenye thamani. Wakati umewadia, siku imefika. Mnunuzi na asifurahi wala muuzaji asihuzunike, kwa maana ghadhabu iko juu ya kundi lote. Muuzaji hatajipatia tena ardhi aliyoiuza wakati wote wawili wangali hai, kwa kuwa maono kuhusu kundi lote hayatatanguka. Kwa sababu ya dhambi zao, hakuna hata mmoja atakayeokoa maisha yake. Watatupa fedha yao barabarani, nayo dhahabu yao itakuwa najisi. Fedha yao na dhahabu yao havitaweza kuwaokoa katika siku hiyo ya ghadhabu ya Bwana. Hawatashibisha njaa yao au kujaza matumbo yao kwa hiyo fedha wala dhahabu, kwa sababu imewaponza wajikwae dhambini. (Ezekieli 7:11-13, 19)
“ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Katika siku ile mawazo yataingia moyoni mwako nawe utapanga mipango mibaya. Utasema, “Nitapigana vita na nchi ambayo vijiji vyake havina maboma. Nitawashambulia watu wanaoishi kwa amani na wasiotarajia vita: wote wanaishi bila maboma na bila malango na makomeo. Nitateka mateka na kuchukua nyara mali za wale waliorudi kuishi katika mahame na wale watu waliokusanywa kutoka kwa mataifa, ambao sasa wana mifugo na mali nyingi, wanaoishi katikati ya nchi.” Sheba na Dedani pamoja na wafanyabiashara wa Tarshishi na vijiji vyake vyote watakuambia, “Je, umekuja kuteka mateka? Je, umekusanya makundi yako ya wajeuri ili kuchukua nyara mali, kutwaa fedha na dhahabu, kutunyangʼanya mifugo na mali na kuteka nyara nyingi zaidi?” ’ (Ezekieli 38:10-13)
Wakati majimbo yaliyo tajiri sana yanajiona salama, atayavamia, naye atafanikisha kile ambacho baba zake wala babu zake hawakuweza. Atagawa nyara, mateka na utajiri miongoni mwa wafuasi wake. Atafanya hila ya kupindua miji yenye maboma, lakini kwa muda mfupi tu. (Danieli 11:24)
Badala ya kuwajali miungu, ataheshimu mungu wa ngome; mungu ambaye hakujulikana na baba zake ndiye atamheshimu kwa dhahabu na fedha, kwa vito vya thamani na zawadi za thamani kubwa. (Danieli 11:38)
Atamiliki hazina za dhahabu, fedha na utajiri wote wa Misri, pamoja na Walibia na Wakushi kwa kujisalimisha. (Danieli 11:43)
Siku ya Bwana inakuja ambayo nyara zilizotekwa kwenu zitagawanywa miongoni mwenu. Nitayakusanya mataifa yote huko Yerusalemu kupigana dhidi yake, mji utatekwa, nyumba zitavamiwa na kuporwa na wanawake watanajisiwa. Nusu ya mji watakwenda uhamishoni, lakini watakaobaki hawataondolewa kutoka mjini. (Zekaria 14:1-2)
Yuda pia atapigana katika Yerusalemu. Utajiri wa mataifa yote yanayoizunguka Yerusalemu utakusanywa, wingi wa dhahabu, fedha na nguo. (Zekaria 14:14)
“Ndivyo ilivyokuwa katika siku za Loti: Watu walikuwa wakila na kunywa, wakinunua na kuuza, wakilima na kujenga. (Luka 17:28)
Lakini yakupasa ufahamu jambo hili, kwamba siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari. Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kumkufuru Mungu, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio watakatifu, (2 Timotheo 3:1-2)
Ndipo nikasikia kile kilichokuwa kama sauti katikati ya wale viumbe wanne wenye uhai ikisema, “Kipimo kimoja cha ngano kwa mshahara wa kibarua wa siku moja, na vipimo vitatu vya shayiri kwa mshahara wa kibarua cha siku moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!” (Ufunuo 6:6)
Ndipo wafalme wa dunia, wakuu wote, majemadari, matajiri, wenye nguvu na kila mtu, mtumwa na mtu huru, wakajificha katika mapango na kwenye miamba ya milima. Wakaiita milima na miamba wakisema, “Tuangukieni, mkatufiche na uso wake yeye aketiye kwenye kiti cha enzi, na mkatuepushe na ghadhabu ya Mwana-Kondoo! (Ufunuo 6:15-16)
Wanadamu waliosalia, ambao hawakuuawa katika mapigo hayo, bado walikataa kutubia kazi za mikono yao na hawakuacha kuabudu mashetani na sanamu za dhahabu, za fedha, za shaba, za mawe na za miti, ambazo haziwezi kuona, kusikia wala kutembea. Wala hawakutubu na kuacha matendo yao ya uuaji, uchawi, uasherati wala wizi wao. (Ufunuo 9:20-21)
Pia alimlazimisha kila mmoja, mdogo na mkubwa, tajiri na maskini, mtu huru na mtumwa, atiwe chapa kwenye mkono wake wa kuume au kwenye kipaji chake cha uso, ili kwamba mtu yeyote asiweze kununua wala kuuza isipokuwa amekuwa na hiyo chapa, ambayo ni jina la huyo mnyama au tarakimu za jina lake. (Ufunuo 13:16-17)
Huyo mwanamke alikuwa amevaa mavazi ya rangi ya zambarau na nyekundu, akimetameta kwa dhahabu, vito vya thamani na lulu. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu kilichojaa mambo ya machukizo na uchafu wa uzinzi wake. (Ufunuo 17:4)
Kwa maana mataifa yote yamekunywa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake. Nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi nao, nao wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na wingi wa utajiri wake.” (Ufunuo 18:3)
“Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumwomboleza kwa sababu hakuna anunuaye bidhaa zao tena: Bidhaa za dhahabu, za fedha, za vito vya thamani na vya lulu, kitani safi, nguo za rangi ya zambarau, hariri, nguo nyekundu, aina zote za miti ya udi, na vifaa vyote vya pembe za ndovu, vifaa vyote vya miti yenye thamani kuliko yote, shaba, chuma na marmar, bidhaa za mdalasini, vikolezi, za uvumba, manemane, na uvumba wenye harufu nzuri, za divai, na mafuta ya zeituni, za unga mzuri na ngano; ngʼombe na kondoo; farasi na magari; na miili na roho za wanadamu. “Watasema, ‘Yale matunda ambayo roho yako iliyatamani yamekoma. Utajiri wako wote na fahari yako vimetoweka, wala haviwezi kupatikana tena kamwe!’ Wale wafanyabiashara waliotajirika kwa bidhaa hizo kutoka kwake watasimama mbali naye kwa hofu kubwa ya mateso yanayompata. Watalia na kuomboleza wakipiga kelele wakisema: “ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa, uliyekuwa umevikwa mavazi ya kitani safi, ya rangi ya zambarau na nyekundu, ukimetameta kwa dhahabu, vito vya thamani na lulu! Katika muda wa saa moja utajiri wote mkubwa kama huu umeangamia!’ “Kila nahodha, na wote wasafirio kwa meli, na wote wapatao kipato chao kutokana na bahari, watasimama mbali. Watakapouona moshi wa kuungua kwake watalia wakisema, ‘Je, kulipata kuwako mji mkubwa kama huu?’ Nao watajirushia mavumbi vichwani mwao, huku wakilia na kuomboleza, wakisema: “ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa, mji ambao wote wenye meli baharini walitajirika kupitia kwa mali zake! Katika saa moja tu ameangamizwa! (Ufunuo 18:11-19)

Watu wadanganyifu kanisani/katika mazingira ya kidini

Kama kweli mkibadili njia zenu na matendo yenu, mkatendeana haki kila mmoja na mwenzake, kama msipomwonea mgeni, yatima wala mjane, na kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, nanyi kama msipofuata miungu mingine kwa madhara yenu wenyewe, ndipo nitawaacha mkae mahali hapa, katika nchi niliyowapa baba zenu milele na milele. Lakini tazama, mnatumainia maneno ya udanganyifu yasiyo na maana. “ ‘Je, mtaiba na kuua, mtazini na kuapa kwa uongo, na kufukiza uvumba kwa Baali, na kufuata miungu mingine ambayo hamkuijua, Je, nyumba hii, iitwayo kwa Jina langu, imekuwa pango la wanyangʼanyi kwenu? Lakini nimekuwa nikiona yanayotendeka! asema Bwana. (Yeremia 7:5-9, 11)
Viongozi wake wanahukumu kwa rushwa, na makuhani wake wanafundisha kwa malipo, nao manabii wake wanatabiri kwa fedha. Hata hivyo wanamwegemea Bwana na kusema, “Je, Bwana si yumo miongoni mwetu? Hakuna maafa yatakayotupata.” (Mika 3:11)
Yesu akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyangʼanyi.” (Mathayo 21:12-13)
Walipofika Yerusalemu, Yesu akaingia katika eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakinunua na kuuza humo ndani. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa, wala hakumruhusu mtu yeyote kuchukua bidhaa kupitia ukumbi wa Hekalu. Naye alipokuwa akiwafundisha, akasema, “Je, haikuandikwa kuwa: “ ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote’? Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyangʼanyi.’ ” (Marko 11:15-17)
Ndipo akaingia eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza vitu humo. Naye akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyangʼanyi.’ ” (Luka 19:45-46)
Huko Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ngʼombe, kondoo na njiwa, nao wengine walikuwa wameketi mezani wakibadili fedha. Akatengeneza mjeledi kutokana na kamba, akawafukuza wote kutoka kwenye eneo la Hekalu, pamoja na kondoo na ngʼombe. Akazipindua meza za wale wabadili fedha na kuzimwaga fedha zao. Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, “Waondoeni hapa! Mnathubutuje kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa biashara?” (Yohana 2:14-16)
Sasa niko tayari kuja kwenu kwa mara hii ya tatu, nami sitawalemea, kwa sababu sitahitaji chochote chenu, ila ninawahitaji ninyi, kwa kuwa hata hivyo watoto hawaweki akiba kwa ajili ya wazazi wao, bali wazazi huweka akiba kwa ajili ya watoto wao. (2 Wakorintho 12:14)
Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha. (1 Timotheo 3:2-3)
Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali. (1 Timotheo 3:8)
...na kuzozana kusikokoma kati ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, na ambao hudhani kwamba utauwa ni njia ya kupata faida. Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa. (1 Timotheo 6:5-6)
Kwa maana wako wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, hasa wale wa kikundi cha tohara. Hao ni lazima wanyamazishwe, kwa sababu wanaharibu watu wa nyumba nzima wakifundisha mambo yasiyowapasa kufundisha. Wanafanya hivyo kwa ajili ya kujipatia mapato ya udanganyifu. (Tito 1:10-11)
Kwa wazee waliomo miongoni mwenu, nawasihi mimi nikiwa mzee mwenzenu, shahidi wa mateso ya Kristo, na mshiriki katika utukufu utakaofunuliwa: lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyowataka mwe; si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumika. (1 Petro 5:1-2)

Mtazamo

Anayependa fedha hatatosheka kamwe

Yeyote apendaye fedha kamwe hatosheki na fedha; yeyote apendaye utajiri kamwe hatosheki na kipato chake. Hili nalo pia ni ubatili. Mali ikiongezeka, ndivyo walaji wanavyoongezeka. Hii nayo inamfaidia nini mwenye mali isipokuwa ni kushibisha macho yake? (Mhubiri 5:10-11)

Mistari mingine

Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, mito haiwezi kuugharikisha. Kama mtu angelitoa mali yote ya nyumbani mwake kwa ajili ya upendo, angelidharauliwa kabisa. (Wimbo 8:7)
...ndivyo itakavyokuwa kwa makuhani na kwa watu, kwa bwana na kwa mtumishi, kwa bibi na kwa mtumishi wake wa kike, kwa muuzaji na kwa mnunuzi, kwa mkopaji na kwa mkopeshaji, kwa mdaiwa na kwa mdai. (Isaya 24:2)
Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana: “Mliuzwa pasipo malipo, nanyi mtakombolewa bila fedha.” (Isaya 52:3)
Jinsi dhahabu ilivyopoteza mngʼao wake, dhahabu iliyo safi haingʼai! Vito vya thamani vimetawanywa kwenye mwanzo wa kila barabara. Wana wa Sayuni wenye thamani, ambao mwanzo uzito wa thamani yao ulikuwa wa dhahabu, sasa wanaangaliwa kama vyungu vya udongo, kazi ya mikono ya mfinyanzi! (Maombolezo 4:1-2)
“Lakini hawakuzingatia, wakaenda zao: huyu shambani mwake na mwingine kwenye biashara zake. (Mathayo 22:5)
Mtu mmoja katika umati wa watu akamwambia Yesu, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane naye urithi wetu.” Lakini Yesu akamwambia, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa hakimu wenu au msuluhishi juu yenu?” Ndipo Yesu akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.” (Luka 12:13-15)
Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Palikuwa na tajiri mmoja na msimamizi wake. Ilisemekana kwamba huyo msimamizi alikuwa anatumia vibaya mali ya tajiri yake. Hivyo huyo tajiri akamwita na kumuuliza, ‘Ni mambo gani haya ninayoyasikia kukuhusu? Toa taarifa ya usimamizi wako, kwa sababu huwezi kuendelea kuwa msimamizi.’ “Yule msimamizi akawaza moyoni mwake, ‘Nitafanya nini sasa? Bwana wangu ananiondoa katika kazi yangu. Sina nguvu za kulima, nami ninaona aibu kuombaomba. Najua nitakalofanya ili nikiachishwa kazi yangu hapa, watu wanikaribishe nyumbani kwao.’ “Kwa hiyo akawaita wadeni wote wa bwana wake, mmoja mmoja. Akamuuliza wa kwanza, ‘Deni lako kwa bwana wangu ni kiasi gani?’ “Akajibu, ‘Galoni 800 za mafuta ya mizeituni.’ “Msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati ya deni lako, ibadilishe upesi, uandike galoni 400.’ “Kisha akamuuliza wa pili, ‘Wewe deni lako ni kiasi gani?’ “Akajibu, ‘Vipimo 1,000 vya ngano.’ “Yule msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati yako, andika vipimo 800!’ “Yule bwana akamsifu yule msimamizi dhalimu kwa jinsi alivyotumia ujanja. Kwa maana watu wa dunia hii wana ujanja zaidi wanapojishughulisha na mambo ya dunia kuliko watu wa nuru. Nawaambia, tumieni mali ya kidunia kujipatia marafiki, ili itakapokwisha, mkaribishwe katika makao ya milele. “Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, pia ni mwaminifu hata katika mambo makubwa, naye mtu ambaye si mwaminifu katika mambo madogo pia si mwaminifu katika mambo makubwa. Ikiwa hamkuwa waaminifu katika mali ya kidunia, ni nani atakayewaaminia mali ya kweli? Nanyi kama hamkuwa waaminifu na mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe? “Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.” Mafarisayo, waliokuwa wapenda fedha, waliyasikia hayo yote na wakamcheka kwa dharau. (Luka 16:1-14)
Simoni alipoona kuwa watu wanapokea Roho Mtakatifu mitume walipoweka mikono juu yao, akataka kuwapa fedha akisema, “Nipeni na mimi uwezo huu ili kila mtu nitakayeweka mikono yangu juu yake apate kupokea Roho Mtakatifu.” Petro akamjibu, “Fedha yako na iangamie pamoja nawe, kwa sababu ulidhani unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha! Wewe huna sehemu wala fungu katika huduma hii kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. Kwa hiyo tubu kwa uovu huu wako na umwombe Bwana. Yamkini aweza kukusamehe mawazo uliyo nayo moyoni mwako. Kwa maana ninaona kwamba wewe umejawa na uchungu na ni mfungwa wa dhambi.” Ndipo Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Bwana, ili hayo mliyosema lolote yasinitukie.” (Matendo 8:18-24)
...kama hata mimi ninavyojaribu kumpendeza kila mtu kwa kila namna. Kwa maana sitafuti mema kwa ajili yangu mwenyewe bali kwa ajili ya wengi, ili waweze kuokolewa. (1 Wakorintho 10:33)
Bali kama watumishi wa Mungu tuonyeshe kwa kila njia: katika saburi nyingi; katika dhiki, katika misiba, na katika shida; tukiwa kama wenye huzuni, lakini siku zote tukifurahi; tukionekana maskini, lakini tukitajirisha wengi; tukiwa kama wasio na kitu, lakini tuna vitu vyote. (2 Wakorintho 6:4, 10)
Basi, kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo alikoketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini mambo yaliyo juu, wala si ya duniani. Kwa maana ninyi mlikufa, nao uhai wenu sasa umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Wakati Kristo, aliye uzima wenu, atakapotokea, ndipo nanyi mtakapotokea pamoja naye katika utukufu. Kwa hiyo, ueni kabisa chochote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: yaani uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ulafi, ambayo ndiyo ibada ya sanamu. (Wakolosai 3:1-5)
Kwa maana kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, wala hakuna kitu chochote cha kukataliwa kama kikipokewa kwa shukrani, (1 Timotheo 4:4)
Mliwahurumia wale waliokuwa kifungoni, mkikubali kwa furaha kunyangʼanywa mali zenu kwa maana mlijua kwamba mnayo mali iliyo bora zaidi idumuyo. (Waebrania 10:34)
Kwa imani, Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. Akachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa kitambo kidogo tu. Aliona kushutumiwa kwa ajili ya Kristo ni utajiri mkubwa zaidi kuliko hazina za Misri, maana alikuwa anatazamia kupata thawabu baadaye. (Waebrania 11:24-26)

Wema licha ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya uovu

Yoabu akamwambia huyo mtu, “Nini! Ulimwona Absalomu? Kwa nini hukumpiga papo hapo mpaka chini? Ndipo ningekupa shekeli kumi za fedha na mkanda wa askari shujaa.” Lakini huyo mtu akamjibu Yoabu, “Hata kama ningepimiwa shekeli 1,000 mikononi mwangu, nisingeinua mkono wangu dhidi ya mwana wa mfalme. Tukiwa tunasikia, mfalme alikuagiza wewe na Abishai pamoja na Itai, akisema, ‘Mlindeni kijana Absalomu kwa ajili yangu.’ (2 Samweli 18:11-12)

Mamluki

Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli siku zote za utawala wao. Mfalme Baasha wa Israeli akashambulia Yuda na kuweka ngome mji wa Rama ili kumzuia yeyote asitoke wala kuingia nchi ya Mfalme Asa wa Yuda. Kisha Asa akachukua fedha yote na dhahabu iliyokuwa imeachwa katika hazina za Hekalu la Bwana na za jumba lake mwenyewe la kifalme. Akawakabidhi maafisa wake na kuwatuma kwa Ben-Hadadi mwana wa Tabrimoni, mwana wa Hezioni, mfalme wa Aramu, aliyekuwa akitawala Dameski. “Akasema na pawepo mkataba kati yangu na wewe, kama ulivyokuwepo kati ya baba yangu na baba yako. Tazama, nimekuletea zawadi ya fedha na dhahabu. Sasa vunja mkataba wako na Baasha mfalme wa Israeli ili aniondokee mimi.” Ben-Hadadi akakubaliana na Mfalme Asa na kutuma majemadari wa majeshi yake dhidi ya miji ya Israeli. Akaishinda miji ya Iyoni, Dani, Abel-Beth-Maaka na Kinerethi yote, pamoja na Naftali. (1 Wafalme 15:16-20)
Kisha Resini mfalme wa Aramu na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli wakaondoka kwenda kupigana dhidi ya Yerusalemu na kumzunguka Ahazi kwa jeshi, lakini hawakuweza kumshinda. Naye Ahazi akachukua fedha na dhahabu zilizopatikana ndani ya Hekalu la Bwana na katika hazina ya jumba la mfalme, na kuzituma kama zawadi kwa mfalme wa Ashuru. Mfalme wa Ashuru akamwitikia kwa kushambulia Dameski na kuiteka. Akawahamishia wenyeji wake huko Kiri, na kumuua Resini. (2 Wafalme 16:5, 8-9)
Ndipo Asa akachukua fedha na dhahabu kutoka hazina ya Hekalu la Bwana na kutoka jumba lake mwenyewe la kifalme na kumpelekea Ben-Hadadi mfalme wa Aramu, ambaye alikuwa anatawala huko Dameski. Akasema, “Pawepo na mkataba kati yangu na wewe, kama ulivyokuwepo kati ya baba yangu na baba yako. Tazama, nimekuletea fedha na dhahabu. Sasa vunja mkataba wako na Baasha mfalme wa Israeli ili aniondokee mimi.” Ben-Hadadi akakubaliana na Mfalme Asa na kutuma majemadari wa majeshi yake dhidi ya miji ya Israeli. Wakashinda Iyoni, Dani, Abel-Maimu na miji yote ya hazina ya Naftali. (2 Nyakati 16:2-4)

Mashtaka mahakamani

Lakini maovu yenu yamewatenga ninyi na Mungu wenu, dhambi zenu zimewaficha ninyi uso wake, ili asisikie. Hakuna hata mmoja anayedai kwa haki; hakuna hata mmoja anayetetea shauri lake kwa haki. Wanategemea mabishano matupu na kusema uongo, huchukua mimba ya magomvi na kuzaa uovu. (Isaya 59:2, 4)
“Patana na mshtaki wako upesi wakati uwapo njiani pamoja naye kwenda mahakamani, ili mshtaki wako asije akakutia mikononi mwa hakimu, naye hakimu akakutia mikononi mwa askari, nawe ukatupwa gerezani. Amin, nakuambia, hautatoka humo hadi uwe umelipa senti ya mwisho. (Mathayo 5:25-26)
Kama mtu akitaka kukushtaki na kuchukua joho lako, mwachie achukue na koti pia. (Mathayo 5:40)
Kama mtu akikupiga shavu moja, mgeuzie na la pili pia. Mtu akikunyangʼanya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia. Mpe kila akuombaye, na kama mtu akichukua mali yako usitake akurudishie. (Luka 6:29-30)
Uwapo njiani na mshtaki wako kwenda kwa hakimu, jitahidi kupatana naye mkiwa njiani. La sivyo, atakupeleka kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa afisa, naye afisa atakutupa gerezani. Nakuambia, hautatoka humo hadi uwe umelipa senti ya mwisho.” (Luka 12:58-59)
Kama mtu yeyote wa kwenu ana ugomvi na mwenzake, anathubutuje kuupeleka kwa wasiomcha Mungu ili kuamuliwa badala ya kuupeleka kwa watakatifu? Je, hamjui kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Nanyi kama mtauhukumu ulimwengu, je, hamwezi kuamua mambo madogo madogo? Hamjui kwamba tutawahukumu malaika? Je, si zaidi mambo ya maisha haya? Kwa hiyo kama kuna ugomvi miongoni mwenu kuhusu mambo kama haya, chagueni kuwa waamuzi, watu ambao wanaonekana hata sio wa heshima katika kanisa. Nasema hivi ili mwone aibu. Je, inawezekana kuwa miongoni mwenu hakuna mtu mwenye hekima ya kutosha kuamua ugomvi kati ya waaminio? Badala yake ndugu mmoja anampeleka mwenzake mahakamani, tena mbele ya watu wasioamini! Huko kuwa na mashtaka miongoni mwenu ina maana kwamba tayari ni kushindwa kabisa. Kwa nini msikubali kutendewa mabaya? Kwa nini msikubali kunyangʼanywa? Badala yake, ninyi wenyewe mwadanganya na kutenda mabaya, tena mwawatendea ndugu zenu. (1 Wakorintho 6:1-8)

Waovu hupinga kazi ya Mungu inapowagharimu fedha

Siku moja, tulipokuwa tukienda mahali pa kusali, tulikutana na mtumwa mmoja wa kike ambaye alikuwa na pepo wa uaguzi. Naye alikuwa amewapa mabwana zake mapato makubwa ya fedha kwa ubashiri. Huyu msichana alikuwa akimfuata Paulo na sisi akipiga kelele, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, wao wanawatangazieni njia ya wokovu.” Akaendelea kufanya hivi kwa siku nyingi, lakini Paulo akiwa ameudhika sana, akageuka na kumwambia yule pepo mchafu, “Ninakuamuru katika jina la Yesu Kristo, umtoke!” Yule pepo mchafu akamtoka saa ile ile. Basi mabwana wa yule mtumwa wa kike walipoona kuwa tumaini lao la kuendelea kujipatia fedha limetoweka, wakawakamata Paulo na Sila wakawaburuta mpaka sokoni mbele ya viongozi wa mji. (Matendo 16:16-19)
Mtu mmoja jina lake Demetrio mfua fedha aliyekuwa akitengeneza vinyago vya fedha vya Artemi na kuwapatia mafundi wake biashara kubwa, aliwaita pamoja watu wengine waliofanya kazi ya ufundi kama yake na kusema, “Enyi watu, mnajua ya kuwa utajiri wetu unatokana na biashara hii! Pia ninyi mmeona na kusikia jinsi ambavyo si huku Efeso peke yake lakini ni karibu Asia yote, huyu Paulo amewashawishi na kuvuta idadi kubwa ya watu kwa kusema kuwa miungu iliyotengenezwa na watu si miungu. Kwa hiyo kuna hatari si kwa kazi yetu kudharauliwa tu, bali pia hata hekalu la mungu mke Artemi, aliye mkuu, anayeabudiwa Asia yote na ulimwengu wote, litakuwa limepokonywa fahari yake ya kiungu.” (Matendo 19:24-27)