Amri ya kutowadhulumu maskini
“Usimtendee mgeni vibaya au kumwonea, kwa kuwa nanyi mlikuwa wageni huko Misri. “Usimdhulumu mjane wala yatima. Kama ukifanya hivyo nao wakinililia, hakika nitasikia kilio chao. Hasira yangu itawaka, nami nitawaua kwa upanga, wake zenu watakuwa wajane na watoto wenu watakuwa yatima. (Kutoka 22:21-24)
Wamesababisha kilio cha maskini kifike mbele zake, hivyo akasikia kilio cha wahitaji. (Ayubu 34:28)
Mtu maskini amwoneaye yeye aliye maskini zaidi ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza mazao. (Mithali 28:3)
Waovu huwadhulumu maskini
Kwa kuwa mpumbavu hunena upumbavu, moyo wake hushughulika na uovu: Hutenda mambo yasiyo ya kumcha Mungu, na hueneza habari za makosa kuhusu Bwana; yeye huwaacha wenye njaa bila kitu, na wenye kiu huwanyima maji. Taratibu za mtu mbaya kabisa ni ovu, hufanya mipango miovu ili kumwangamiza maskini kwa uongo, hata wakati ambapo hoja za mhitaji ni za haki. (Isaya 32:6-7)
Maelezo ya watu wanaowadhulumu maskini
Kama simba angurumaye au dubu ashambuliaye, ndivyo alivyo mtu mwovu atawalaye wanyonge. (Mithali 28:15)
...wale ambao meno yao ni panga na ambao mataya yao yamewekwa visu kuwaangamiza maskini katika nchi, na wahitaji kutoka miongoni mwa wanadamu. (Mithali 30:14)
Hukumu juu ya wanaowadhulumu maskini
Watoto wake watalipa yote baba yao aliyowadhulumu maskini, nayo mikono yake itarudisha mali yote aliyonyangʼanya watu. (Ayubu 20:10)
Atatema mali alizozimeza; Mungu atalifanya tumbo lake kuzitapika. (Ayubu 20:15)
Vile alivyovitaabikia atavirudisha bila kuvila; hatafurahia faida itokanayo na biashara yake. Kwa kuwa aliwaonea maskini na kuwaacha pasipo kitu; amenyangʼanya kwa nguvu nyumba asizozijenga. “Hakika hatakuwa na raha katika kutamani kwake sana; hawezi kujiokoa mwenyewe kwa hazina zake. (Ayubu 20:18-20)
...giza nene linavizia hazina zake. Moto usiopepewa na mtu utamteketeza, na kuangamiza yaliyosalia nyumbani mwake. (Ayubu 20:26)
Mafuriko yataichukua nyumba yake, maji yaendayo kasi katika siku ya ghadhabu ya Mungu. (Ayubu 20:28)
Waovu huchomoa upanga na kupinda upinde, ili wawaangushe maskini na wahitaji, kuwachinja wale ambao njia zao ni nyofu. Lakini panga zao zitachoma mioyo yao wenyewe, na pinde zao zitavunjwa. (Zaburi 37:14-15)
Mtu anayemdai na ateke vyote alivyo navyo, matunda ya kazi yake yatekwe nyara na wageni. (Zaburi 109:11)
Kwa maana kamwe hakuweza kutenda wema, bali alimfukuza mnyonge na mhitaji, aliwafanyia jeuri wahitaji na waliovunjika moyo. (Zaburi 109:16)
Yeye amwoneaye maskini ili kujiongezea mali, naye ampaye tajiri zawadi, wote huwa maskini. (Mithali 22:16)
Usiwadhulumu maskini kwa sababu ni maskini, wala kumdhulumu mhitaji mahakamani, kwa sababu Bwana atalichukua shauri lao naye atawateka wao waliowateka. (Mithali 22:22-23)
Bwana anaingia katika hukumu dhidi ya wazee na viongozi wa watu wake: “Ninyi ndio mlioharibu shamba langu la mizabibu, mali zilizonyangʼanywa maskini zimo nyumbani mwenu. Mnamaanisha nini kuwaponda watu wangu na kuzisaga nyuso za maskini?” asema Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote. (Isaya 3:14-15)
Ole wao wawekao sheria zisizo za haki, kwa wale watoao amri za kuonea, kuwanyima maskini haki zao na kuzuilia haki za watu wangu walioonewa, kuwafanya wajane mawindo yao na kuwanyangʼanya yatima. (Isaya 10:1-2)
Hili ndilo asemalo Bwana: “Shuka kwenye jumba la kifalme la mfalme wa Yuda, utangaze ujumbe huu huko: ‘Sikia neno la Bwana, ee mfalme wa Yuda, wewe uketiye kwenye kiti cha enzi cha Daudi: wewe, maafisa wako na watu wako mnaopitia malango haya. Hili ndilo Bwana asemalo: Tenda haki na adili. Mwokoe mkononi mwa mdhalimu yeye aliyetekwa nyara. Usimtendee mabaya wala ukatili mgeni, yatima au mjane, wala usimwage damu isiyo na hatia mahali hapa. Kwa kuwa ukiwa mwangalifu kushika maagizo haya, ndipo wafalme watakaokalia kiti cha enzi cha Daudi watakapoingia kupitia malango ya jumba hili la kifalme, wakiwa wamepanda magari na farasi, huku wakifuatana na maafisa wao na watu wao. Lakini kama hutayatii maagizo haya, asema Bwana, ninaapa kwa nafsi yangu kwamba jumba hili litakuwa gofu.’ ” (Yeremia 22:1-5)
Ndani yako wamewadharau baba na mama, ndani yako wamewatendea wageni udhalimu na kuwaonea yatima na wajane. (Ezekieli 22:7)
Watu wa nchi wanatoza kwa nguvu na kufanya unyangʼanyi, wanawatenda jeuri maskini na wahitaji na kuwaonea wageni, wakiwanyima haki. (Ezekieli 22:29)
Hili ndilo asemalo Bwana: “Kwa dhambi tatu za Israeli, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Wanawauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu. Wanakanyaga juu ya vichwa vya maskini, kama vile juu ya mavumbi ya nchi, na kukataa haki kwa walioonewa. Baba na mwanawe hushiriki msichana mmoja, kwa hivyo hulinajisi Jina langu takatifu. (Amosi 2:6-7)
Sikilizeni neno hili, ninyi ngʼombe wa Bashani mlioko juu ya Mlima Samaria, ninyi wanawake mnaowaonea maskini, na kuwagandamiza wahitaji, na kuwaambia wanaume wenu, “Tuleteeni vinywaji!” Bwana Mwenyezi ameapa kwa utakatifu wake: “Hakika wakati utakuja mtakapochukuliwa na kulabu, na wanaosalia kwa ndoana za samaki. (Amosi 4:1-2)
...yeye hufanya maangamizo kwenye ngome na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa), mnamchukia yule akemeaye mahakamani, na kumdharau yule ambaye husema kweli. Mnamgandamiza maskini na kumlazimisha awape nafaka. Kwa hiyo, ingawa mmejenga majumba ya mawe ya fahari, hamtaishi ndani yake; ingawa mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu, hamtakunywa divai yake. Kwa kuwa ninajua hesabu ya makosa yenu na ukubwa wa dhambi zenu. Mmewaonea wenye haki na kupokea rushwa na kuzuia haki ya maskini mahakamani. (Amosi 5:9-12)
Lisikieni hili, ninyi ambao mnawagandamiza wahitaji, na kuwaonea maskini wa nchi, mkisema, “Ni lini Mwezi Mwandamo utakapopita ili tupate kuuza nafaka, na Sabato itakwisha lini ili tuweze kuuza ngano?” Mkipunguza vipimo, na kuongeza bei, na kudanganya kwa mizani zisizo sawa, mkiwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu, na mkiuza hata takataka za ngano pamoja na ngano. (Amosi 8:4-6)
“Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Fanyeni hukumu za haki, onyesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi. Msimwonee mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’ “Lakini wakakataa kusikiliza, wakanipa kisogo kwa ukaidi na kuziba masikio yao. Wakaifanya mioyo yao migumu kama jiwe gumu na hawakuisikiliza sheria au maneno ambayo Bwana Mwenye Nguvu Zote aliyatuma kwa njia ya Roho wake kupitia manabii waliotangulia. Kwa hiyo Bwana Mwenye Nguvu Zote alikasirika sana. (Zekaria 7:9-12)
“Basi nitakuja karibu nanyi ili kuhukumu. Nami nitakuwa mwepesi kushuhudia dhidi ya wachawi, wazinzi, waapao kwa uongo, wanaopunja vibarua malipo yao, wanaowaonea wajane na yatima, na wanaowanyima wageni haki, lakini hawaniogopi mimi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. (Malaki 3:5)
Ombi kwamba Bwana ahukumu dhuluma dhidi ya maskini
Ee Mhukumu wa dunia, inuka, uwalipize wenye kiburi kama wanavyostahili. (Zaburi 94:2)
Wanamchinja mjane na mgeni, na kuwaua yatima. (Zaburi 94:6)
Nao husema, “Bwana haoni, Mungu wa Yakobo hafahamu.” (Zaburi 94:7)
Mfano wa kuwadhulumu maskini
Katika nguo zako watu huona damu ya uhai ya maskini wasio na hatia, ingawa hukuwakamata wakivunja nyumba. Lakini katika haya yote (Yeremia 2:34)
Watu wa kidini wanaowadhulumu maskini
Alipokuwa akifundisha, Yesu alisema, “Jihadharini na walimu wa sheria. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa kwa heshima masokoni. Pia wao hupenda kukaa kwenye viti vya mbele katika masinagogi, na kupewa nafasi za heshima katika karamu. Wao hula nyumba za wajane, na ili waonekane kuwa wema wanasali sala ndefu. Watu kama hawa watapata hukumu iliyo kuu sana.” (Marko 12:38-40)
“Jihadharini na walimu wa sheria. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa kwa heshima masokoni. Hupenda kukaa kwenye viti vya mbele katika masinagogi, na kukaa kwenye nafasi za heshima katika karamu. Wao hula nyumba za wajane, na ili waonekane kuwa wema, wanasali sala ndefu. Watu kama hawa watapata hukumu iliyo kuu sana.” (Luka 20:46-47)
Kuwadhulumu maskini ni jambo la kawaida
Kama ukiona maskini wanaonewa katika nchi, hukumu na haki vikipotoshwa, usishangazwe na mambo hayo, kwa maana afisa mmoja anaangaliwa na aliye juu yake zaidi na juu ya hao wawili kuna wengine walio juu zaidi yao. (Mhubiri 5:8)
Watetee/wasaidie maskini/wasio na msaada
“Sema kwa ajili ya wale wasioweza kujisemea, kwa ajili ya haki za wote walioachwa ukiwa. Sema na uamue kwa haki, tetea haki za maskini na wahitaji.” (Mithali 31:8-9)
...jifunzeni kutenda mema! Tafuteni haki, watieni moyo walioonewa. Teteeni shauri la yatima, wateteeni wajane. (Isaya 1:17)
Ewe nyumba ya Daudi, hili ndilo Bwana asemalo: “ ‘Hukumuni kwa haki kila asubuhi, mwokoeni mikononi mwa mdhalimu yeye aliyetekwa nyara, la sivyo ghadhabu yangu italipuka na kuwaka kama moto kwa sababu ya uovu mlioufanya: itawaka na hakuna wa kuizima. (Yeremia 21:12)
Wanaomcha Mungu huwasaidia maskini
Mwenye haki hujali haki kwa ajili ya maskini, bali mwovu hajishughulishi na hilo. (Mithali 29:7)
Je, sikulia kwa ajili ya wale waliokuwa katika taabu? Je, nafsi yangu haikusononeka kwa ajili ya maskini? (Ayubu 30:25)
Bwana huwabariki wanaowasaidia maskini
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Heri mtu yule anayemjali mnyonge, Bwana atamwokoa wakati wa shida. Bwana atamlinda na kuyahifadhi maisha yake, atambariki katika nchi na hatamwacha katika tamaa ya adui zake. Bwana atamtegemeza awapo mgonjwa kitandani, atamwinua kutoka kitandani mwake. (Zaburi 41:1-3)
Yeye amhurumiaye maskini humkopesha Bwana, naye atamtuza kwa aliyotenda. (Mithali 19:17)
Alimbariki kiongozi aliyewasaidia maskini
Kama mfalme akiwaamua maskini kwa haki, kiti chake cha enzi kitakuwa thabiti siku zote. (Mithali 29:14)
Kama kweli mkibadili njia zenu na matendo yenu, mkatendeana haki kila mmoja na mwenzake, kama msipomwonea mgeni, yatima wala mjane, na kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, nanyi kama msipofuata miungu mingine kwa madhara yenu wenyewe, ndipo nitawaacha mkae mahali hapa, katika nchi niliyowapa baba zenu milele na milele. Lakini tazama, mnatumainia maneno ya udanganyifu yasiyo na maana. “ ‘Je, mtaiba na kuua, mtazini na kuapa kwa uongo, na kufukiza uvumba kwa Baali, na kufuata miungu mingine ambayo hamkuijua, (Yeremia 7:5-9)
Walishe maskini na Bwana atakulipa
Kisha Yesu akamwambia yule aliyewaalika, “Uandaapo karamu ya chakula cha mchana au cha jioni, usialike rafiki zako au ndugu zako au jamaa zako au majirani zako walio matajiri tu. Ukifanya hivyo, wao nao wanaweza kukualika kwao, nawe ukawa umelipwa kile ulichofanya na kupata thawabu yako. Bali ufanyapo karamu, waalike maskini, vilema na vipofu, nawe utabarikiwa kwa sababu hawa hawana uwezo wa kukulipa. Mungu atakulipa wakati wa ufufuo wa wenye haki.” Mmoja wa wale waliokuwa pamoja naye mezani aliposikia hivi akamwambia Yesu, “Amebarikiwa mtu yule atakayekula katika karamu ya Ufalme wa Mungu!” Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anaandaa karamu kubwa, akaalika watu wengi. Wakati wa karamu ulipofika, akamtuma mtumishi wake akawaambie wale walioalikwa, ‘Karibuni, kila kitu ki tayari sasa.’ “Lakini wote, kila mmoja, wakaanza kutoa udhuru: Wa kwanza akasema, ‘Nimenunua shamba, lazima niende kuliona. Tafadhali niwie radhi.’ “Mwingine akasema, ‘Ndipo tu nimenunua jozi tano za ngʼombe wa kulimia, nami ninakwenda kuwajaribu, tafadhali niwie radhi.’ Naye mwingine akasema, ‘Nimeoa mke, kwa hiyo siwezi kuja.’ “Yule mtumishi akarudi, akampa bwana wake taarifa. Ndipo yule mwenye nyumba akakasirika, akamwagiza yule mtumishi wake, akisema, ‘Nenda upesi kwenye mitaa na vichochoro vya mjini uwalete maskini, vilema, vipofu na viwete.’ “Yule mtumishi akamwambia, ‘Bwana, yale uliyoniagiza nimefanya, lakini bado ipo nafasi.’ “Ndipo yule bwana akamwambia mtumishi wake, ‘Nenda kwenye barabara na vijia vilivyoko nje ya mji na uwalazimishe watu waingie ili nyumba yangu ipate kujaa. (Luka 14:12-23)
Mhukumu maskini kwa haki
“Usiwanyime haki watu wako walio maskini katika mashtaka yao. (Kutoka 23:6)
Usipotoshe hukumu ya mgeni au yatima, au kuchukua vazi la mjane kama rehani. (Kumbukumbu 24:17)
Wahurumie maskini
Wewe utafukuzwa mbali na wanadamu, nawe utaishi pamoja na wanyama pori; utakula manyasi kama ngʼombe, na kuloana kwa umande wa mbinguni. Nyakati saba zitapita juu yako, mpaka utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme za wanadamu, naye humtawaza yeyote amtakaye. Amri ya kuacha kisiki pamoja na mizizi yake inamaanisha kwamba ufalme wako utarejezwa kwako utakapokubali kwamba Mbingu ndizo zitawalazo. Kwa hiyo, ee mfalme, uwe radhi kupokea shauri langu: Acha dhambi zako kwa kutenda yaliyo haki, ukaache uovu wako, na uwe na huruma kwa walioonewa. Hivyo itawezekana baada ya hayo, mafanikio yako yakaendelea.” (Danieli 4:25-27)
Wasiowatetea maskini watahukumiwa
Kama vitundu vilivyojaa ndege, nyumba zao zimejaa udanganyifu; wamekuwa matajiri na wenye nguvu, wamenenepa na kunawiri. Matendo yao maovu hayana kikomo; hawatetei mashauri ya yatima wapate kushinda, hawatetei haki za maskini. Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya hili?” asema Bwana. “Je, nisijilipizie kisasi juu ya taifa kama hili? (Yeremia 5:27-29)
Dhambi ya Sodoma: kutowasaidia maskini
“ ‘Sasa hii ilikuwa ndiyo dhambi ya dada yako Sodoma: yeye na binti zake walikuwa na majivuno, walafi na wazembe, hawakuwasaidia maskini na wahitaji. (Ezekieli 16:49)
Mfano wa kiongozi asiyewatetea maskini
Watawala wenu ni waasi, rafiki wa wevi, wote wanapenda rushwa na kukimbilia hongo. Hawatetei yatima, shauri la mjane haliletwi mbele yao lisikilizwe. (Isaya 1:23)
Jinsi tunavyowatendea maskini huakisi juu ya Bwana
Yeye amwoneaye maskini huonyesha dharau kwa Muumba wao, bali yeyote anayemhurumia mhitaji humheshimu Mungu. (Mithali 14:31)
Yeye anaye mdhihaki maskini huonyesha dharau kwa Muumba wake; yeyote afurahiaye maafa hataepuka kuadhibiwa. (Mithali 17:5)
Sehemu ya Mungu kwa maskini
Bwana huwaruzuku/huwalinda maskini na wahitaji
Huwapigania yatima na wajane, humpenda mgeni, akimpa chakula na mavazi. (Kumbukumbu 10:18)
Humwokoa mhitaji kutokana na upanga ulioko kinywani mwao; huwaokoa kutokana na makucha ya wenye nguvu. (Ayubu 5:15)
Lakini mhitaji hatasahaulika siku zote, wala matumaini ya walioonewa hayatapotea. (Zaburi 9:18)
Lakini wewe, Ee Mungu, unaona shida na huzuni, umekubali kuyapokea mkononi mwako. Mhanga anajisalimisha kwako, wewe ni msaada wa yatima. (Zaburi 10:14)
“Kwa sababu ya uonevu wa wanyonge na kulia kwa uchungu kwa wahitaji, nitainuka sasa,” asema Bwana. “Nitawalinda kutokana na wale wenye nia mbaya juu yao.” (Zaburi 12:5)
Maskini huyu alimwita Bwana, naye akamsikia, akamwokoa katika taabu zake zote. (Zaburi 34:6)
Nitapaza sauti yangu nikisema, “Ni nani aliye kama wewe, Ee Bwana? Wewe huwaokoa maskini kutokana na wale walio na nguvu kuliko wao, maskini na mhitaji kutokana na wanaowanyangʼanya!” (Zaburi 35:10)
Lakini bado mimi ni maskini na mhitaji; Bwana na anifikirie. Wewe ndiwe msaada wangu na Mwokozi wangu; Ee Mungu wangu, usikawie. (Zaburi 40:17)
Mungu huwaweka wapweke katika jamaa, huwaongoza wafungwa wakiimba, bali waasi huishi katika nchi kame. (Zaburi 68:6)
Ee Mungu, watu wako waliishi huko, nawe kwa wingi wa utajiri wako uliwapa maskini mahitaji yao. (Zaburi 68:10)
Bwana huwasikia wahitaji wala hadharau watu wake waliotekwa. (Zaburi 69:33)
Ataitikia maombi ya mtu mkiwa, wala hatadharau hoja yao. (Zaburi 102:17)
Baadhi yao walitangatanga jangwani, hawakuona njia ya kuwafikisha mji ambao wangeweza kuishi. (Zaburi 107:4)
Kwa maana husimama mkono wa kuume wa mhitaji, kuokoa maisha yake kutoka kwa wale wanaomhukumu. (Zaburi 109:31)
Huwainua maskini kutoka mavumbini, na kuwanyanyua wahitaji kutoka kwenye jalala, (Zaburi 113:7)
Nitambariki kwa kumpa mahitaji tele: nitashibisha maskini wake kwa chakula. (Zaburi 132:15)
Najua kwamba Bwana huwapatia maskini haki, na kuitegemeza njia ya mhitaji. (Zaburi 140:12)
Naye huwapatia haki walioonewa na kuwapa wenye njaa chakula. Bwana huwaweka wafungwa huru, (Zaburi 146:7)
Bwana huwalinda wageni na kuwategemeza yatima na wajane, lakini hupinga njia za waovu. (Zaburi 146:9)
Bwana huwahifadhi wanyenyekevu lakini huwashusha waovu mpaka mavumbini. (Zaburi 147:6)
Bwana hubomoa nyumba ya mtu mwenye kiburi, bali huilinda mipaka ya mjane isiguswe. (Mithali 15:25)
...bali kwa uadilifu atahukumu wahitaji, kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia. Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu. (Isaya 11:4)
Maskini kuliko maskini wote watapata malisho, nao wahitaji watalala salama. Lakini mzizi wako nitauangamiza kwa njaa, nayo njaa itawaua walionusurika. (Isaya 14:30)
Umekuwa kimbilio la watu maskini, kimbilio la mhitaji katika taabu yake, hifadhi wakati wa dhoruba na kivuli wakati wa hari. Kwa maana pumzi ya wakatili ni kama dhoruba ipigayo ukuta (Isaya 25:4)
“Maskini na wahitaji wanatafuta maji, lakini hayapo, ndimi zao zimekauka kwa kiu. Lakini Mimi Bwana nitawajibu, Mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha. (Isaya 41:17)
Mwimbieni Bwana! Mpeni Bwana sifa! Yeye huokoa uhai wa mhitaji kutoka mikononi mwa waovu. (Yeremia 20:13)
Ombi kwamba Bwana awasaidie maskini
Atawatetea walioonewa miongoni mwa watu na atawaokoa watoto wa wahitaji, ataponda mdhalimu. Wafalme wa Tarshishi na wa pwani za mbali watamletea kodi; wafalme wa Sheba na Seba watampa zawadi. Kwa maana atamwokoa mhitaji anayemlilia, aliyeonewa asiye na wa kumsaidia. Atawahurumia wanyonge na wahitaji na kuwaokoa wahitaji kutoka mauti. Atawaokoa kutoka uonevu na ukatili, kwani damu yao ni ya thamani machoni pake. Aishi maisha marefu! Na apewe dhahabu ya Sheba. Watu wamwombee daima na kumbariki mchana kutwa. (Zaburi 72:4, 10, 12-15)
Usiruhusu walioonewa warudi nyuma kwa aibu; maskini na wahitaji hebu walisifu jina lako. (Zaburi 74:21)
Teteeni wanyonge na yatima, tunzeni haki za maskini na walioonewa. Mwokoeni mnyonge na mhitaji, wakomboeni kutoka mkononi mwa mwovu. (Zaburi 82:3-4)
Lakini wewe, Ee Bwana Mwenyezi, unitendee wema kwa ajili ya jina lako, uniokoe kwa wema wa pendo lako. Maana mimi ni maskini na mhitaji, moyo wangu umejeruhiwa ndani yangu. (Zaburi 109:21-22)
Mtazamo wa wanadamu juu ya sehemu ya Mungu na maskini
Watu husogeza mawe ya mpaka; huchunga makundi ya wanyama waliyonyangʼanya kwa nguvu. Huwanyangʼanya yatima punda wao, na kumchukua rehani fahali wa mjane. Humsukuma mhitaji kutoka njia, na kuwafanya maskini wote wa nchi kulazimika kujificha. Kama punda-mwitu jangwani, maskini huzunguka katika kazi zao za kutafuta chakula; mahali palipo jangwa huwapa chakula cha watoto wao. Hukusanya chakula mashambani na kuokota masazo katika mashamba ya mizabibu ya waovu. Kwa kukosa nguo, usiku kucha hukaa uchi; hawana chochote cha kujifunika baridi. Hutota kwa mvua za mlimani, nao huikumbatia miamba kwa ajili ya kukosa pa kujisitiri. Mtoto yatima hupokonywa matitini; mtoto wachanga wa maskini hunyakuliwa kwa ajili ya deni. Kwa kukosa nguo, hutembea uchi; hubeba miganda ya ngano, lakini huwa na njaa. Hukamua zeituni katika mawe ya kusagia; hukanyaga mashinikizo, lakini wanaona kiu. Kilio cha huzuni cha wanaokufa kinapaa kutoka mjini, nazo nafsi za waliojeruhiwa zinalilia msaada. Lakini Mungu hamlaumu mtu yeyote kwa kutenda mabaya. Wakati mwanga wa mchana unapotoweka, muuaji huinuka naye huwaua maskini na mhitaji; wakati wa usiku hunyemelea kama mwizi. (Ayubu 24:2-12, 14)
Mtazamo wa Mungu juu ya maskini
Naijua dhiki yako na umaskini wako, lakini wewe ni tajiri! Nayajua masingizio ya wale wasemao kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali wao ni sinagogi la Shetani. (Ufunuo 2:9)
Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu chochote.’ Lakini hutambui ya kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi. Nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, ili upate kuwa tajiri, na mavazi meupe ili uyavae upate kuficha aibu ya uchi wako, na mafuta ya kupaka macho yako ili upate kuona. (Ufunuo 3:17-18)
Bwana aliwachagua wanyonge ili kuwaaibisha wenye nguvu
Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika jamaa zenye vyeo. Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima, Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu. (1 Wakorintho 1:26-27)
Bwana aliwaumba watu wote
Tajiri na maskini wanafanana kwa hili: Bwana ni Muumba wao wote. (Mithali 22:2)
Mtu maskini na mtu anayeonea wanafanana kwa jambo hili: Bwana hutia nuru macho yao wote wawili. (Mithali 29:13)
Mtazamo wa wanadamu juu ya maskini
Mtu mwenye hekima ana faida gani zaidi ya mpumbavu? Mtu maskini anapata faida gani kwa kujua jinsi ya kujistahi mbele ya watu wengine? (Mhubiri 6:8)
Matatizo na faida kwa maskini
Matatizo ya maskini
Maskini wana marafiki wachache
Maskini huepukwa hata na majirani zao, bali matajiri wana marafiki wengi. (Mithali 14:20)
Mali huleta marafiki wengi, bali rafiki wa mtu maskini humwacha. (Mithali 19:4)
Mtu maskini huepukwa na ndugu zake wote: Je, marafiki zake watamkwepa kiasi gani! Ingawa huwafuata kwa kuwasihi, hawapatikani popote. (Mithali 19:7)
Maskini huteseka kwa dhuluma
Shamba la mtu maskini laweza kuzalisha chakula kingi, bali dhuluma hukifutilia mbali. (Mithali 13:23)
Maskini huongea na matajiri kwa unyenyekevu
Mtu maskini huomba kuhurumiwa bali tajiri hujibu kwa ukali. (Mithali 18:23)
Maskini huwatumikia matajiri
Matajiri huwatawala maskini naye akopaye ni mtumwa wa akopeshaye. (Mithali 22:7)
Maskini hupuuzwa
Palikuwa na mji mdogo uliokuwa na watu wachache ndani yake. Mfalme mwenye nguvu akainuka dhidi yake, akauzunguka akaweka jeshi kubwa dhidi yake. Katika mji huo kulikuwepo mtu mmoja maskini lakini mwenye hekima, naye akauokoa ule mji kwa hekima yake. Lakini hakuna aliyemkumbuka yule maskini. Kwa hiyo, nikasema, “Hekima ni bora kuliko nguvu.” Lakini hekima ya maskini imedharauliwa, wala hakuna anayesikiliza maneno yake. (Mhubiri 9:14-16)
Umaskini
Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome, bali ufukara ni maangamizi ya maskini. (Mithali 10:15)
Ombi la kutokuwa maskini
“Ninakuomba vitu viwili, Ee Bwana; usininyime kabla sijafa: Uutenge mbali nami udanganyifu na uongo; usinipe umaskini wala utajiri, bali unipe chakula cha kunitosha kila siku. Nisije nikawa na vingi vya kuzidi nikakukana na kusema, ‘Bwana ni nani?’ Au nisije nikawa maskini nikaiba, nami nikaliaibisha jina la Mungu wangu. (Mithali 30:7-9)
Faida kwa maskini
Maskini wanaitwa heri
Akawatazama wanafunzi wake, akasema: “Mmebarikiwa ninyi mlio maskini, kwa sababu Ufalme wa Mungu ni wenu. (Luka 6:20)
“Lakini ole wenu ninyi mlio matajiri, kwa sababu mmekwisha kupokea faraja yenu. (Luka 6:24)
Maskini ni matajiri katika imani
Ndugu zangu, sikilizeni: Je, Mungu hakuwachagua wale walio maskini machoni pa ulimwengu kuwa matajiri katika imani na kuurithi Ufalme aliowaahidi wale wampendao? (Yakobo 2:5)
Maskini wanahubiriwa Injili
Roho wa Bwana Mwenyezi yu juu yangu, kwa sababu Bwana amenitia mafuta kuwahubiria maskini habari njema. Amenituma kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao; (Isaya 61:1)
Yohana aliposikia akiwa gerezani mambo ambayo Kristo alikuwa akiyafanya, aliwatuma wanafunzi wake ili wakamuulize, “Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?” Yesu akajibu, “Rudini mkamwambie Yohana yale mnayosikia na kuyaona: Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema. (Mathayo 11:2-5)
“Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa sababu amenitia mafuta kuwahubiria maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaweka huru wanaoonewa, (Luka 4:18)
Hivyo akawajibu wale wajumbe, “Rudini mkamwambie Yohana yote mnayoyaona na kuyasikia: Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa habari njema. (Luka 7:22)
Maskini hawatatekwa nyara kwa ajili ya mali
Utajiri wa mtu waweza kukomboa maisha yake, bali mtu maskini hasikii kitisho. (Mithali 13:8)
Maskini wanaomjua Bwana watafarijiwa mbinguni
“Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, ambaye aliishi kwa anasa kila siku. Hapo penye mlango wake aliishi maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima. Huyo Lazaro alitamani kujishibisha kwa makombo yaliyoanguka kutoka mezani kwa yule tajiri. Hata mbwa walikuwa wakija na kuramba vidonda vyake. “Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Abrahamu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa. Kule kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa karibu yake. Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Abrahamu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu.’ “Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu. (Luka 16:19-25)
Maskini wanaweza kujivunia kuwa watoto wa Mungu
Ndugu asiye na cheo kikubwa yampasa ajivunie hali hiyo maana ametukuzwa. Lakini yeye aliye tajiri afurahi kwa kuwa ameshushwa, kwa sababu atatoweka kama ua la shambani. (Yakobo 1:9-10)
Wakati wa kurejeshwa kwa Israeli, maskini watanufaika
Mara nyingine tena wanyenyekevu watafurahi katika Bwana, wahitaji watafurahi katika yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli. (Isaya 29:19)
Maskini mwenye hekima humtambua tajiri
Mtu tajiri anaweza kuwa na hekima machoni pake mwenyewe, bali mtu maskini mwenye ufahamu atamfichua. (Mithali 28:11)
Mambo ambayo umaskini ni bora kuliko hayo
Afadhali mtu maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama, kuliko mpumbavu ambaye midomo yake imepotoka. (Mithali 19:1)
Lile mtu alionealo shauku ni upendo usio na mwisho, afadhali kuwa maskini kuliko kuwa mwongo. (Mithali 19:22)
Afadhali maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama kuliko tajiri ambaye njia zake ni potovu. (Mithali 28:6)
Mifano ya maskini
Watumishi wa Sauli wakarudia hayo maneno kwa Daudi. Lakini Daudi akasema, “Je, mnafikiri ni jambo dogo kuwa mkwewe mfalme? Mimi ni mtu maskini tu, na nisiyejulikana sana.” (1 Samweli 18:23)
Lakini bado mimi ni maskini na mhitaji; Ee Mungu, unijie haraka. Wewe ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu; Ee Bwana, usikawie. (Zaburi 70:5)
Maombi ya Daudi. Ee Bwana, sikia na unijibu, kwa maana mimi ni maskini na mhitaji. (Zaburi 86:1)
Watu wake wote wanalia kwa uchungu watafutapo chakula; wanabadilisha hazina zao kwa chakula ili waweze kuendelea kuishi. “Tazama, Ee Bwana, ufikiri, kwa maana nimedharauliwa.” (Maombolezo 1:11)
Ulipotimia wakati wa utakaso wake Maria kwa mujibu wa Sheria ya Mose, basi Yosefu na Maria walimpeleka mtoto Yerusalemu, ili kumweka wakfu kwa Bwana (kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana, kwamba, “Kila mtoto wa kiume kifungua mimba atawekwa wakfu kwa Bwana”), na pia kutoa dhabihu kulingana na yale yaliyonenwa katika Sheria ya Bwana: “Hua wawili au makinda mawili ya njiwa.” (Luka 2:22-24)
Mpaka saa hii tuna njaa na kiu, tu uchi, tumepigwa na hatuna makao. Tunafanya kazi kwa bidii kwa mikono yetu wenyewe. Tunapolaaniwa, tunabariki, tunapoteswa, tunastahimili, (1 Wakorintho 4:11-12)
Bali kama watumishi wa Mungu tuonyeshe kwa kila njia: katika saburi nyingi; katika dhiki, katika misiba, na katika shida; katika kupigwa, katika kufungwa gerezani na katika ghasia; katika kazi ngumu, katika kukesha na katika kufunga; tukiwa kama wenye huzuni, lakini siku zote tukifurahi; tukionekana maskini, lakini tukitajirisha wengi; tukiwa kama wasio na kitu, lakini tuna vitu vyote. (2 Wakorintho 6:4-5, 10)
Nimekuwa katika kazi ngumu na taabu, katika kukesha mara nyingi; ninajua kukaa njaa na kuona kiu; nimefunga kula chakula mara nyingi; nimehisi baridi na kuwa uchi. (2 Wakorintho 11:27)
Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Lakini, mlifanya vyema kushiriki nami katika taabu zangu. (Wafilipi 4:11-14)
Maskini/matajiri kanisani
Kwanza, mnapokutana kama kanisa, nasikia kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwenu, nami kwa kiasi fulani nasadiki kuwa ndivyo ilivyo. Bila shaka lazima pawe na tofauti miongoni mwenu ili kuonyesha ni nani anayekubaliwa na Mungu. Mkutanikapo pamoja si chakula cha Bwana mnachokula, kwa kuwa mnapokula, kila mmoja wenu anakula bila kuwangoja wengine. Mmoja hukaa njaa na mwingine analewa. Je, hamna nyumbani kwenu ambako mnaweza kula na kunywa? Au mnalidharau kanisa la Mungu na kuwadhalilisha wale wasio na kitu? Niwaambie nini? Je, niwasifu juu ya jambo hili? La, hasha! (1 Wakorintho 11:18-22)
Kuwapa maskini
Kurudishwa kwa ardhi
Mwaka wa hamsini utakuwa yubile kwenu, msipande wala msivune kile kiotacho chenyewe, au kuvuna zabibu zisizohudumiwa. Kwa kuwa ni yubile, nayo itakuwa takatifu kwenu; mtakula tu kile kilichotoka moja kwa moja mashambani. “ ‘Katika huu Mwaka wa Yubile, kila mmoja atarudi kwenye mali yake mwenyewe. (Walawi 25:11-13)
Sheria kuhusu maskini waliokuwa watumwa
“ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini katikati yako, naye akajiuza kwako, usimfanye atumike kama mtumwa. Atatendewa kama mfanyakazi aliyeajiriwa, au kama mkazi wa muda katikati yako, naye atatumika mpaka Mwaka wa Yubile. Ndipo yeye na watoto wake wataachiwa, naye atarudi kwa watu wa ukoo wake, na kwenye mali ya baba zake. Kwa sababu Waisraeli ni watumishi wangu niliowaleta kutoka nchi ya Misri, kamwe wasiuzwe kama watumwa. Usiwatawale kwa ukatili, lakini utamcha Mungu wako. “ ‘Watumwa wako wa kiume na wa kike watatoka katika mataifa yanayokuzunguka; kutoka kwao waweza kununua watumwa. Pia waweza kununua baadhi ya wakazi wa muda wanaoishi katikati yako, na jamaa ya koo zao waliozaliwa katika nchi yako, nao watakuwa mali yako. Hao waweza kuwarithisha watoto wako kuwa urithi wao, na wanaweza kuwafanya watumwa maisha yao yote, lakini usiwatawale ndugu zako Waisraeli kwa ukatili. “ ‘Ikiwa mgeni au mkazi wa muda katikati yako atakuwa tajiri, na mmoja wa wazawa wa nchi yako akawa maskini, naye akajiuza kwa yule mgeni anayeishi katikati yako, au kwa mmoja wa jamaa wa koo za wageni, anayo haki ya kukombolewa baada ya kujiuza. Mmoja wa jamaa zake aweza kumkomboa: Mjomba wake, au binamu yake, au yeyote aliye ndugu wa damu katika ukoo wake aweza kumkomboa. Au ikiwa atafanikiwa, anaweza kujikomboa mwenyewe. Yeye na huyo aliyemnunua watahesabu muda kuanzia mwaka aliojiuza hadi Mwaka wa Yubile. Mahali pa kuanzia bei ya kuachiwa kwake itakadiriwa kwa ujira unaolipwa mfanyakazi aliyeajiriwa kwa idadi ya hiyo miaka. Ikiwa imebaki miaka mingi, ni lazima atalipia ukombozi wake fungu kubwa la bei iliyolipwa kumnunua yeye. Ikiwa miaka iliyobaki ni michache kufikia Mwaka wa Yubile, atafanya hesabu yake, naye atalipa malipo yanayostahili kwa ajili ya ukombozi wake. Atatendewa kama mtu wa kuajiriwa mwaka hadi mwaka; lazima uone kwamba yule aliyemnunua hamtawali kwa ukatili. “ ‘Hata ikiwa hakukombolewa kwa njia mojawapo ya hizi, yeye na watoto wake wataachiwa katika Mwaka wa Yubile, (Walawi 25:39-54)
Kutotii sheria kulileta hukumu
“Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Nilifanya agano na baba zenu nilipowatoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. Nilisema, ‘Kila mwaka wa saba, kila mmoja wenu ni lazima amwache huru mtumwa ambaye ni Mwebrania mwenzenu aliyejiuza kwenu. Baada ya kukutumikia kwa miaka sita, ni lazima umwache huru aende zake.’ Hata hivyo baba zenu hawakunisikiliza wala kunijali. Hivi karibuni tu mlitubu na kufanya yaliyo sawa machoni pangu: Kila mmoja wenu aliwatangazia uhuru Waebrania wake. Hata mlifanya agano mbele zangu ndani ya nyumba iitwayo kwa Jina langu. Lakini sasa mmegeuka na kulinajisi jina langu. Kila mmoja wenu amemrudisha mtumwa wa kiume na wa kike ambao mlikuwa mmewaacha huru waende zao walikotaka. Mmewalazimisha kuwa watumwa wenu tena. “Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana: Hamkunitii mimi. Hamkutangaza uhuru kwa ndugu zenu. Hivyo sasa, ninawatangazia ninyi ‘uhuru,’ asema Bwana: ‘uhuru’ ili kuanguka kwa upanga, tauni na njaa. Nitawafanya mwe chukizo kwa falme zote za dunia. (Yeremia 34:13-17)
Mengineyo
Mambo yanayomfanya mtu kuwa maskini
Yeye anayedharau maonyo hupata umaskini na aibu, bali yeye anayekubali maonyo huheshimiwa. (Mithali 13:18)
Usiupende usingizi la sivyo utakuwa maskini, uwe macho nawe utakuwa na chakula cha akiba. (Mithali 20:13)
Mtu apendaye anasa atakuwa maskini, yeyote apendaye mvinyo na mafuta kamwe hatakuwa tajiri. (Mithali 21:17)
Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo, au wale walao nyama kwa pupa, kwa maana walevi na walafi huwa maskini, nako kusinzia huwavika matambara. (Mithali 23:20-21)
Pasingekuwa na maskini nchini kama watu wangetii kikamilifu
Hata hivyo, hapatakuwepo maskini miongoni mwenu, kwa kuwa katika nchi Bwana Mungu wenu anayowapa kuimiliki kama urithi wenu, atawabariki sana, ikiwa tutamtii Bwana Mungu wenu kikamilifu na kuwa waangalifu kuyafuata maagizo haya yote ninayowapa leo. (Kumbukumbu 15:4-5)
Maskini peke yao ndio walioachwa katika nchi iliyoshindwa
Akawachukua watu wa Yerusalemu wote kwenda uhamishoni: yaani maafisa wote na mashujaa, watu wenye ustadi na ufundi, jumla yao watu elfu kumi. Watu maskini sana ndio tu waliobaki katika nchi. (2 Wafalme 24:14)
Lakini yule jemadari wa askari walinzi akawaacha baadhi ya wale watu maskini kabisa ili watunze mashamba ya mizabibu na mashamba mengine. (2 Wafalme 25:12)
Lakini Nebuzaradani kiongozi wa walinzi aliwabakiza baadhi ya watu maskini katika nchi ya Yuda, ambao hawakuwa na kitu. Naye wakati huo akawapa mashamba ya mizabibu na mashamba mengine. (Yeremia 39:10)
Maafisa wote wa jeshi na watu wao waliokuwa bado wapo kwenye eneo la wazi waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemteua Gedalia mwana wa Ahikamu kuwa mtawala wa nchi, na amemweka kuwa kiongozi wa wanaume, wanawake na watoto waliokuwa maskini zaidi katika nchi ambao hawakuchukuliwa kwenda uhamishoni Babeli, (Yeremia 40:7)
Nebuzaradani, jemadari wa askari walinzi, akawapeleka uhamishoni baadhi ya watu maskini sana na wale waliobaki katika mji, pamoja na mabaki ya watu wa kawaida, na wale waliojisalimisha kwa mfalme wa Babeli. (Yeremia 52:15)